Friday, January 29, 2010

Mwanza waipania Simba

Na Jacqueline Massano

KAMANDA wa Polisi wa mkoa wa Mwanza, Jamal Rwambow amesema iwe isiwe ni lazima timu ya Toto African iifunge Simba ili kujinusuru isishuke daraja kutokana na kuwa na pointi chache kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayoendelea kwenye vituo mbalimbali.
Simba inayoongoza kwenye msimamo wa Ligi kwa kuwa na pointi 39 inatarajia kushuka dimbani kesho kumenyana na Toto kwenye mechi inayotarajia kufanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Kamanda Rwambow alisema kutokana na jitihada walizozifanya za wananchi kuichangishia timu hiyo ili isishuke daraja ana imani inaweza kuifunga Simba siku hiyo ya Jumapili.
"Simba haiwezi kutoka Mwanza, iwe isiwe ni lazima ifungwe tu. Haiwezekani ije Mwanza halafu iondoke na ushindi huku kwetu," alisema Kamanda huyo ambaye pia ni shabiki mkubwa wa Simba.
Rwambow alisema kama timu hiyo iliweza kuifunga Simba msimu uliopita ilipoenda kucheza Mwanza, na sasa hivi wanataka kuendelea kuifunga tena. "Mzunguko wa kwanza ilitufunga kwa sababu ilikuwa Dar lakini nawaambia hivi tutawafunga tena. Ni kweli mimi naipenda Simba lakini ni lazima tuifunge," alisema
Alisema juhudi zote hizo ni kuinusuru timu hiyo ili iweze kucheza ligi kuu na kuwafanya wakazi wa Mwanza waweze kuziona timu za Simba na Yanga zikienda Mwanza kucheza soka na wala si vinginevyo.
"Tukifanya mchezo wakazi wa Mwanza watakuwa hawazioni tena timu za Simba na Yanga, na ndiyo maana na wenyewe waliamua kuichangia na kuisaidia Toto pale ilipokwama na hii yote ni kuitaka timu yao ibaki kwenye ligi," alisema
Alisema kwa sasa timu yao ina pointi nane kwenye msimamo wa ligi, kutokana na hali hiyo watafanya juhudi ili iliweze kushinda mechi zake zote saba ambazo anachezea nyumbani. "Tuna mechi saba nyumbani, hizi ni lazima tushinde, na tukishinda zote tutakuwa na pointi 28 hivyo itakuwa si rahisi kushuka daraja tena," alisema
Kamanda huyo alisema ikiwa itashindikana na timu ikashuka daraja watakuwa hawana jinsi itabidi waombe radhi kwa wakazi wa Mwanza na kujipanga upya ili timu iweze kupanda daraja tena.

No comments:

Post a Comment