Sunday, January 3, 2010

Stars vs Ivory Coast leo

#Wadau waitabiria makubwa Stars

WADAU mbalimbali wa soka nchini, wameitabiria timu yao ya taifa, Taifa Stars itajifunza mambo mengi ya kisoka pale itakapocheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya 'Tembo' wa Ivory Coast. Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa soka nchini, itafanyika katika uwanja wa Taifa saa 1.30 usiku.
Mshauri wa timu ya soka ya Villa Squad ya Dar, Kenneth Mwaisabula, alisema mechi hiyo ni fursa nzuri kwa wachezaji wa Stars kujifunza mambo mengi kutoka kwa wapinzani wao.
"Ivory Coast ina wachezaji wengi wa kulipwa, wanafahamu mbinu mbalimbali za soka, hivyo vijana wetu wanatakiwa kuwa makini na kuangalia makosa yao ili waweze kujifunza toka kwa wenzao," alisema Mwaisabula.
Alisema mechi dhidi ya timu kubwa zenye wachezaji wa kulipwa, ni nzuri kwa timu zetu kwa kuchukua mbinu na mafunzo toka kwao na kuepukana na soka la kizamani.
mdau mwingine wa soka, Nassor Duduma katibu msaidizi wa zamani wa Yanga, alisema mechi ya leo ina malengo tofauti kwa wachezaji wa timu zote mbili huku Ivory Coast ikiwa katika maandalizi ya fainali za mataifa ya Afrika huko Angola na Stars kujifunza.
"Stars lengo lake katika mechi hiyo ni kuonyesha wanaweza na kujifunza kwa kupambana na Drogba (Didier) na Toure (Kolo), lakini wageni wanaangalia zaidi katika fainali za kule Angola," alisema Duduma.
Wakati Duduma akisema hayo, mdau mwingine wa Jijini Mwanza, Jamal Rwambow, alisema mchezo wa leo ni muhimu kwa Stars kwa sababu utatoa nafasi ya wachezaji wetu kujifunza mengi.
"Siwapi nafasi Ivory Coast ya kutushinda, lakini naamini tunaweza kutoka sare ama kushinda mechi hiyo," alisema Rwambow ambaye ni Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza.
Aidha, alisema wachezaji wa Stars wanatakiwa kujiamini na kucheza bila woga na kuweza kuepuka majina ya wachezaji wakubwa wanaocheza soka Ulaya.
Hata hivyo, kocha maarufu nchini, Syllersaid Mziray, alipotakiwa kuzungumzia mechi hiyo, alisema kwa ufupi "Sina la kuzungumza".
Mziray ambaye amekuwa akiipinga mechi hiyo kwa madai Stars haitajifunza lolote, safari hii ameonekana kuwa mkimya zaidi.

No comments:

Post a Comment