Monday, July 13, 2009

uchawi kwenye soka

Mchezaji wa kigeni afichua ushirikina ulivyogubika soka la Tanzania


Na Jacqueline Massano
MASUALA ya ushirikina katika soka ya nchi yetu ingawa yamekuwa yakizungumziwa kichinichini lakini kwa kweli kwa miaka mingi sasa yameonekana kushamiri katika soka ya nchi yetu.

Uchawi katika soka kwa kiasi kikubwa umekuwa hauzungumziwi waziwazi kutokana na sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa imani ikiwa suala hilo litazumgumzwa basi mtoa siri anaweza kudhurika.

Hata hivyo, kuna watu wachache waliokuwa na ubavu na kujitokeza waziwazi kuelezea jinsi, ambayo suala hilo lilivyo baya na linavyodumaza akili za wanasoka wetu.

Kutokana na ukweli kuwa basi kama kweli uchawi ungekuwa unafanya kazi basi timu ya soka ya taifa, Taifa Stars ingekuwa mabingwa wa dunia, Afrika lakini ushahidi wa suala hilo uko kwenye rekodi za michuano ya kimataifa.

Kama kweli suala hilo lingekuwa kuna nguvu katika soka basi kwa nini Simba, Yanga na timu nyingine zinaboronga kwenye mechi za kimataifa?

Imani za ushirikina, hata hivyo, limekuwa likiwekewa kipaumbele kuanzia soka ya ngazi za chini hadi kwenye ngazi ya taifa.

Mashabiki wa soka nchini kwa miaka mingi wamekuwa wakishuhudia vitendo mbalimbali vinavyoashiria soka yetu kugubikwa na imani za uchawi.

Hali hiyo ya imani za ushirikina imekuwa ikitawala kwa muda mrefu, ambao zaidi na hushuhudiwa kabla ya mechi za soka kuanza.

Kwa mfano kuna timu huamua kuruka ukuta wa uwanja kabla ya mechi kwa kuhofia pengine kutakuwa uchawi wa kuwadhuru kwenye geti la kuingilia uwanjani.

Kuna nyakati nyingine wachezaji huingia uwanjani bila ya kufunga kamba za viatu na kufungia uwanjani.

Hata hivyo, katika miaka ya 1980, kulikuwa kuna matumizi ya ndege aina ya njiwa kama ilivyotokea katika mechi ya Simba na Yanga mwaka 1981, ambapo mashabiki wa Simba walirusha njiwa aliyefungwa hirizi na baadae alishindwa kuruka kutoka uwanjani.

Pia bila ya kusahau vitendo vya kuvunja mayai uwanjani, ambavyo vimekuwa vikifanyika mara nyingi katika soka.

Kwa mfano mwaka 1974 wakati mshambuliaji wa Simba, Saad Ally alipoanguka katika mchezo dhidi ya Yanga, ambao Simba ililala 2-1 kwenye uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza kumekuwa kuna imani kwa hadi leo hii kuwa pale alipoangukia Saad hakuna jani lililoota hadi.

Mchezaji mmoja kigeni, ambaye anachezea timu mojawapo kubwa ya jijini Dar es Salaam na aliomba kuhifadhiwa jina lake kwa kuhofia kuzodolewa, alieleza ushirikina imekuwa sehemu ya maisha ya klabu hiyo anayochezea.

Alisema anaamini sababu kubwa inayofanya klabu za soka nchini kuliporomosha soka la Tanzania ni pamoja na wachezaji wake kujikita katika imani za uchawi.

Alisema imefikia wakati sasa uchawi umeingia katika damu za viongozi na wachezaji wa klabu kiasi cha kushindwa kuwaamini wachezaji wake na kuamua kuwapeleka kwa mganga ili waweze kuibuka na ushindi viwanjani.

Klabu hizo zinaamini haziwezi kufanya vizuri bila ya kujihusisha na masuala ya ushirikiana ikiwa ni pamoja na kwenda kwa mganga ili ziweze kupewa dawa ya ushindi.

Mchezaji huyo sio wa kwanza kulalamikia suala hilo, hata kocha wa zamani wa Yanga, marehemu Tambwe Leya aliwahi kulalamikia suala hilo wakati alipokuwa anainoa Yanga katika vipindi tofauti.

Tambwe mara ya kwanza alipokuja kufundisha Yanga katika miaka ya 1970, moja ya masuala, ambayo aliyapiga vita kwa kiasi kikubwa yalikuwa masuala ya uchawi katika soka.

Kocha, ambaye alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na muumini mkubwa wa kanisa la Katoliki, alifikia hatua kukorofishana na uongozi wa Yanga kutokana na masuala hayo.

Aliingia katika ugomvi mkubwa mwaka 1975, wakati wa maandalizi ya mechi ya robo fainali ya Klabu Bingwa ya Afrika dhidi ya Enugu Rangers ya Nigeria.

Yanga ilitolewa kwa sheria ya ugenini baada ya kufungana 1-1 jijini, Dar es Salaam lakini timu hizo zilikuwa zimeshindwa kufungana katika mchezo wa kwanza jijini Enugu.

Tambwe, hata hivyo, alilalamikia kuwa kitendo cha viongozi wa Yanga kuwafanyisha kwa muda mrefu masuala ya ushirikina na kuwafanya kushindwa kuzingatia mafunzo yake.

Pia mwaka 1995, aliporejea kuinoa Yanga kwa mara ya pili ilijikuta ikitolewa na Blackpool ya Zimbabwe kwenye robo fainali ya Kombe la Washindi baada ya kufungwa mechi zote mbili, Tambwe alilalamikia kitendo cha wachezaji kuamshwa usiku wa manane.

Mwaka 1996, Yanga kulifumuka mgogoro mkubwa wa matumizi mabaya ya fedha za Kombe la Hedex baada ya kudaiwa kuwa viongozi walitumia kiasi cha sh. milioni 3.3 kwa masuala ya ushirikina.

Pia Simba kumekuwa na kawaida ya kuchagua viongozi walio na uwezo wa kuifunga Yanga na hasa kwenye masuala ya ushirikina na sio katika masuala ya uongozi wa soka.

Ndio maana hata viongozi wa zamani wa Simba wamekuwa wakizungumziwa kwa sifa zaidi ya kuifunga Yanga na sio masuala ya kuendeleza klabu.

Kwa mfano kumekuwa kuna msemo kuwa Pan African imekuwa ikipanda na kushuka kutoka kwenye ligi kutokana na `kumzika fedha' mganga wao aliyewasaidia kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara na ule wa Muungano mwaka 1982.


Vitendo hivyo vya kishirikina si kwa Tanzania pekee hata kwa nchi za Afrika ambazo zinaamini kuwa ushirikina ni moja ya silaha ya mafanikio katika soka na si vinginevyo.

Hata hivyo, ushirikina huo haupo tu kwa klabu kwani hata wachezaji nao wanaamini kuwa hawawezi kucheza soka uwanjani bila ya kufanya mambo ya kichawi kama vile kwenda kwa mganga kwa ajili ya kupewa kinga.

Mchezaji huyo alifichua hata baadhi ya wachezaji majina yao (tunayahifadhi) wanatuhumiwa kujihusisha na masuala ya kishirikina ikiwa ni pamoja na kusaka njia za kuwafanya wenzao wasicheze soka.

Wachezaji hao wanaamini hakuna kitu cha ziada ambacho kinaweza kutumika bila kukubali kujishughulisha na suala hilo la ubebaji wa 'matunguli' na ndiyo njia pekee ya kupata namba.

Pia alilalamia kuwa wachezaji wengi wa Tanzania hawaamini kucheza mpira bila ya kujihusisha na masuala ya ushirikina. Imani hiyo inawafanya baadhi yao kudiriki hata kuwaumiza wenzao kwa kuwaendea kwa waganga.

Kuna msemo wachezaji wengi huwa wanapenda kuutumua kuwa fulani amempigilia 'misuli' mwenzake ili achukue namba yake. Huu msemo unatumika sana kwenye soka hasa kwa baadhi ya wachezaji wenye tabia hizo za kishirikina.

Akizungumzia kuhusiana na suala hilo la ushirikina mmoja wa wachezaji wa klabu kubwa hapa nchini, anasema suala hilo la ushirikina lipo na amelishuhudia kwa macho yake kutoka kwa wachezaji na viongozi wa klabu hizo akifichua wakati hirizi ziliposhonwa katika jezi zao.

Alieleza baada ya kuona kitu hicho aligoma kuvaa jezi hiyo na baadae aligomea kitendo cha kupelekwa katika kambi ya maficho kwa ajili ya kufanya ushirikina wa kujihami kufungwa.

Mchezaji huyo anasema yeye binafsi haamini kama ushirikina ni moja ya njia mbadala ya kumfanya aweze kuwika katika medani ya soka. "Mimi binafsi siamini uchawi kwani nimekulia katika dini, inakuwa ni vigumu kuamini vitu kama hivyo.

"Kwa kweli tukiendelea hivi sidhani kama tutafika mbali, kwani wachezaji wengi wa kitanzania wanapenda sana ushirikina. Na hii inatokana na baadhi yao kutojiamini kama wanaweza," anasema mshambuliaji huyo wa kimataifa.

Anasema tangu amejiunga na timu hiyo mkubwa hapa nchini, amekutana na mambo mengi ya kutisha ambayo yanahusishwa na uchawi na hakuamini kama yanaweza kufanywa na klabu kubwa kama hiyo. "Siyo tu wachezaji, hata viongozi wanaamini kuwa hawawezi kupeleka timu uwanjani hadi waende kwa waganga," alisema.

Anafafanua kuwa wachezaji wakiona hawapangwi katika mechi huwa wanakimbilia kwa waganga kwa ajili ya kuelezea shida zao, kitu ambacho anadai si suluhisho katika soka.

"Kupangwa au kutopangwa kwenye mechi ni suala la kocha, na wala si kwenda kwa mganga kuomba msaada. Pia wanatakiwa wakumbuke kuwa juhudi ndiyo zinakufanya kocha akuone na kukupanga na wala si mganga." anasema kwa masikitiko.

Anaongeza kuwa wachezaji wengi wa Tanzania ni wavivu wa mazoezi na wala hawajitumi uwanjani na ndiyo maana wanapoona hawapangwi katika mechi wanaanza kuhisi kuwa fulani kamroga na yeye anaamua kwenda kwa mganga.

Kutokana na hali hiyo, mshambuliaji huyo anasema wachezaji wa aina hiyo mara nyingi huwa wanazeekea kwenye timu zao kwa sababu hawawezi kwenda kucheza soka popote pale kufuatia na imani zao za kishirikina.

Alisema kwa kiasi kikubwa hali hiyo imechangia wanasoka wengi kushindwa kupata nafasi ya kucheza Ulaya kutokana na kutokuwa fiti.

"Ulaya hakuna uchawi kwenye soka, kule ni vipaji tu. Na ndiyo maana hakuna mchezaji hata mmoja ambaye anaweza kupata timu nje, yote ni kwa sababu ya uchawi tu," anaongeza

Akitolea mfano wa timu za nje, anasema wachezaji wengi wa nje wanajituma kwenye mazoezi na wanashika kile wanachofundishwa na ndiyo maana wanawika na wala si masuala ya ushirikina.

"Ushirikiano ndiyo kitu pekee kwa wachezaji, siyo mwingine anawaza ushirikina mwingine anategea uwanjani kitu ambacho hakipo kabisa kwenye soka," alieleza.

Anasema ameshuhudia mara kadhaa viongozi wakizipeleka timu kwa waganga ili ziweze kufanya vizuri lakini haikusaidia kitu na matokeo yake timu inachapwa mabao mengi. "Haya sasa yule anayekwenda kwa mganga na asiyekwenda kwa mganga yupi bora?" alihoji mchezaji huyo.

"Hapa kinachotakiwa ni mbinu tu na wala si kupeleka wachezaji kwa waganga, huko hakuna mafanikio hata kidogo," anamalizia kwa kusema

Licha ya kauli hizo kutoka kwa mchezaji, klabu za Simba na Yanga mara kwa mara zimehusishwa katika matukio mbalimbali ya ushirikina hasa timu hizo mbili zinapokuwa zinakutana.

Pia baadhi ya wazee wa klabu hizo mbili wanaamini kuwa kwa kufanya hivyo, timu inaweza kufanya vizuri na kuibuka kwa ushindi na ndio maana huomba hata bajeti kubwa kwa sababu ya masuala hayo ambayo wameyabatiza kuwa ya `utendaji'.

====

No comments:

Post a Comment