Thursday, October 29, 2009

Akudo yatema wanenguaji wengine

Na Sabato Kasika, Jijini

BENDI ya Akudo 'Vijana wa Masauti, imeendelea na zoezi la kuwatema wanenguaji wake ambapo sasa wale waliorudishwa nyumbani kwao Kongo wamefikia watano.
Awali waliorudishwa kwa mara ya kwanza kutokana na kiwango chao cha kazi kushuka walikuwa watatu na sasa wameongezeka wengine wawili na kufanya idadi yao kuwa watano.
Meneja wa bendi hiyo Fadhil Mfate aliwataja waliotemwa awali kuwa ni Judith, Cerren na Shushuu ambapo wameongezeka wengine wawili aliowataja kwa majina ya Joseline na Fanny Bosawa.
"Nafasi hawa wawili zimeshachulikuwa na Bekham na Sandra ambao tayari wameshaanza kuonyesha makali yao ndani ya bendi ya Akudo Impact," amesema Mfate.
Amefafanua kuwa nafasi za wale watatu wa awali zitazibwa siku chache zijazo kwa madai kwamba kuna mtu ambaye uongozi wa bendi umemtuma Kongo kuleta wanenguaji wapya.
Amesema kabla ya kumtuma mtu kuwaleta, kulikuwa na mpango ambao walikubaliana na Werason kwamba angekuja kufanya onyesho nchini na kisha kuiachia Akudo wanenguaji watatu.
Amedai kuwa kwa vile bendi hiyo iko matawi ya juu, inataka wanenguaji wenye viwango ambao watasaidia kuifanya iendelee kubaki kwenye nafasi hiyo ambayo inang'ang'aniwa na bendi nyingi.
Wakati ikiendelea na maandalizi ya albamu ya pili, Akudo inatamba na nyimbo za albamu ya kwanza ya Impact ambazo baadhi yake ni 'Safari Sio Kifo', 'Walimwengu sio Binadamu', 'Yako Wapi Mapenzi'.

No comments:

Post a Comment