Tuesday, December 1, 2009

Chokolaa atimuliwa Twanga Pepeta

Na Abdul Mitumba
UONGOZI wa African Stars Entertainment Tanzania 'ASET', umemtimua kazi mwimbaji wake, Khalidi Chokolaa aliyekuwa katika bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Mkurugenzi mtendaji wa ASET, Asha Baraka amesema wameamua kumtimua Chokolaa baada ya kubaini kutaka kuigawa bendi hiyo baada ya kuanzisha bendi nyingine kivyake.
"Tumebaini njama alizokuwa akizifanya kwa muda mrefu, awali tulidhani lengo lake la kuanzisha kundi akiwa ndani ya Twanga lililenga kujiongezea kipato, lakini baadaye tukabaini lengo ni kutaka kuisambatarisha bendi yetu," amesema.
Hata hivyo, Asha amesema hatua zilizochukuliwa na ASET dhidi ya Chokolaa ni ya muda na kwamba endapo ataachana na kundi lake, wapo tayari kumrejesha kundini kwa sababu ASET bado inamhitaji.
Uamuzi wa ASET kumtimua Chokolaa umefuatia akiwa na wenzake watatu wa Twanga kuiasi bendi na kuanzisha kundi jipya la Mapacha Wanne wakimshirikisha msanii mmoja wa bendi ya FM Academia.
Awali meneja wa ASET, Abuu Semhando alisema mbali na Chokolaa waimbaji wengine ni Kalala Junior na Charlz Baba wakati yule wa FM Academia akiwa ni Jose Mara.
"Huu ni sawa na uasi, kama wataendelea kung'ang'ania kundi lao hilo ni bora waachane na Twanga ili nafasi zao zichukuliwe na wanamuziki wengine haraka kadri itakavyowezekana," amesema Semhando.
Hata hivyo, hadi jana ni Chokolaa pekee ndiye hakuwepo Twanga huku wengine wote wakishiriki maonyesho yote likiwemo bonanza la kila Jumapili pale Leaders Club, Kinondoni.

No comments:

Post a Comment