Tuesday, December 1, 2009

Madega aifagilia Yanga

Na Daniel Mkate
HUKU ikiwa imefanya usajili wa wachezaji wawili tu katika dirisha dogo, mwenyekiti anayemaliza muda wake katika klabu ya Yanga , Iman Madega, amesema atahakikisha anapoondoka madarakani anaiacha klabu hiyo kwenye mstari mzuri.
Awali Yanga ilipanga kufanya uchaguzi wake mkuu Januari 3 mwakani, lakini kutokana na Shirikisho la Soka nchini kusitisha zoezi hilo kwa klabu hadi Jan.15, huenda sasa ukafanya katikati ya mwezi huo.
Madega alisema baada ya timu yake kuwasajili wachezaji wawili wa kimataifa kutoka Kenya na Ghana, anaamini itafanya vyema katika mzunguko wa pili wa ligi kuu huku ikiwa inashika nafasi ya tatu katika msimamo mzima wa ligi hiyo.
"Tumefanya usajili mzuri ingawa ni wa wachezaji wawili tu, kipa Yaw Berko kutoka Liberty Professionals FC ya Ghana na John Njoroge kutoka Kenya...tumejipanga vyema zaidi mzunguko wa pili," alisema Madega.
Madega alisema pamoja na kuwa hatowania tena uongozi Yanga, lakini atahakikisha anaiacha klabu hiyo katika hali nzuri kutokana na uongozi uliojengeka wa viongozi wenzake.
"Viongozi watakaochukua klabu watakuta timu ipo katika hali nzuri, itafanya mazuri katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo inayotarajiwa kuanza katika ya Januari mwakani," alisema.
Katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Yanga imekuwa ikienda mwendo wa kuasuasua tofauti na mahasimu wao Simba wanaoongoza ligi kwa pointi 33 baada ya kushinda mechi zote 11 walizocheza huku Yanga wakiwa na pointi 21 tu.

No comments:

Post a Comment