Monday, November 16, 2009

Diego 'jela' miezi 2

ZURICH, Uswisi
KOCHA wa timu ya taifa ya Argentina, Diego Maradona amefungiwa kutojishughulisha na soka kwa muda wa miezi miwili na kutozwa faini zaidi ya shilingi milioni 24 kufuatia kauli alizotoa wakati wa mechi ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Afrika Kusini.
Maradona, 49, aliomba radhi kwa kauli alizotoa, kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, FIFA.
Maradona anatuhumiwa kutoa maneno machafu wakati akihojiwa 'live' na kituo cha televisheni wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Kocha huyo aliyechaguliwa kufundisha timu ya taifa ya Argentina miezi 13 iliyopita baada ya muda mrefu wa ushauri na matibabu ya kuacha kutumia dawa za kulevya na ulezi wa pombe, aliitwa na kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu ya FIFA.
"Kamati ya nidhamu ya FIFA leo hii imeamua kumpa adhabu ya miezi miwili kutojihusisha na soka na faini ya shilingi milioni 24 kocha wa timu ya taifa ya Argentina Diego Maradona," ilisema taarifa ya FIFA.
"Kamati imetupilia mbali ombi la msamaha la Maradona.
"Kamati imeonya, endapo Maradona atarudia tena utovu wa nidhamu kama huo, ina maana kwamba atakabiliwa na adhabu zaidi."FIFA imesema adhabu hiyo inaanza mara moja na kwamba itamalizika Januari 15.
Hii ina maana kwamba, Maradona hatakosa mechi za mashindano, bali atakuwa ndani ya adhabu wakati kikosi chake kikicheza na timu ya taifa ya Czech katika mechi ya kirafiki mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment