Monday, November 16, 2009

Yanga: Nurdin aendi popote

UONGOZI wa klabu ya soka ya Yanga, umedai mchezaji wao kiungo Nurdin Bakari, hawana mpango wa kumtoa kwa timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu Bara kutokana na mkataba wake wa miaka miwili kutomalizika.
Afisa Habari wa timu hiyo, Louis Sendeu, amesema licha ya habari zilizoenea Jijini kuwa mchezaji huyo anafukuziwa na Simba, lakini uongozi wa wana Jangwani hauna mpango wa kumtoa.
"Iwapo Simba wanamuhitaji mchezaji huyo wasifanye papara za kuzungumza naye, kwani bado ana mkataba nasi kwa kipindi cha miaka miwili ijayo, hivyo wasikurupuke kama wamempata Mike Barasa ni huyo huyo wala si Nurdin," alisema Sendeu.
Sendeu alisema mchezaji huyo kwa hivi sasa hana mpango na Simba kutokana na kumuacha katika usajili miaka miwili iliyopita kwa kile kilichoelezwa matatizo ya moyo.
"Kwa sasa Simba wamesahau kama walimuacha mchezaji huyo kwa sababu ya matatizo ya moyo, sasa iweje waanze kumnyatia tena," alihoji msemaji huyo.
Habari zinasema baada ya Simba kufanikiwa kumnasa mchezaji Mkenya, Mike Barasa, kwa sasa wamemgeukia kiungo huyo ili kuimarisha kikosi chao katika dirisha dogo la usajili baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kumalizika leo wakati Yanga itakapocheza na Prisons ya Mbeya.
Hata hivyo, Sendeu alisema iwapo Simba wanamtamani mchezaji huyo, wanatakiwa kuwasiliana na uongozi wa klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani ili kufanya mazungumzo ya 'kujenga'.
Mchezaji huyo alivutiwa na aliyekuwa kocha mserbia wa Yanga, Dusan Kondic, licha ya matatizo yake ya moyo yaliyodaiwa na Simba, hata kumshawishi kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo kumuita katika kikosi chake.

No comments:

Post a Comment