Friday, November 20, 2009

JK 'amuua' Tenga

Na Daniel Mkate, U/Taifa
BAADA ya kuteta kirafiki na Rais wa Shirikisho la Soka nchini, TFF, Leodger Tenga, kabla hajapanda jukwaani kulipokea Kombe la Dunia, Rais Jakaya Kikwete, 'alimuua' bila aibu kiongozi huyo wa soka kuhususiana na mwenendo wa shirikisho lake.
Akizungumza baada ya kupewa nafasi kuhutubia shamrashamra za kulikaribisha kombe hilo, JK alisema TFF limeonekana kuwa shirikisho la ushabiki na mapato pekee yake badala ya kuendeleza soka.
"Ulegevu wa TFF ni ushabiki na mapato pekee, sijui inakuwaje katika kuendeleza soka nchini...mwenendo huu ukiendelea hivi lazima tutadumaa na tutaendelea kusimamia ligi kuu pekee," alisema JK na kumuacha Tenga akifurahi shingo upande.
JK alisema pamoja na shirikisho hilo kuonekana kuendeshwa kwa misingi hiyo, lakini bado limeonekana la kipekee ulimwenguni kwa kutoa adhabu za kukomoa wachezaji.
"Naona ajabu sana, mchezaji akifanya kosa anafungiwa miezi sita, jamani hizo adhabu mmezitoa wapi...kwanini asifungiwe mechi tatu na fani juu yake, tunahitajai vijana wetu wacheze soka na si kukomoana," alishangaa JK.
Pamoja na kulishukia shirikisho hilo, pia JK alizipiga dongo klabu kubwa nchi za Simba na Yanga kuhusiana na kutojenga misingi ya soka la vijana na kukimbilia kushindana kununua wachezaji kwa bei mbaya.
Alisema soka la vijana ndio msingi mkubwa, lakini klabu zetu hizi kubwa (bila kuzitaja) zisiogopwe pale TFF inapojenga misingi yake.
"Klabu jengeni vipaji , tuwekeze katika soka la umri mdogo...tafuteni walimu wazuri na wala si wachambuzi wa soka ili kuendeleza soka," alisema.
Kombe la Dunia lipo nchini kwa ziara ya siku tatu ambayo inamalizika rasmi kesho huku pia wakazi wa visiwa vya Unguja wakipata nafasi ya kuliona.

No comments:

Post a Comment