Friday, November 13, 2009

kauli zamponza Fergie, atupwa selo

LONDON, England
KOCHA wa Manchester United, Alex Ferguson amelimwa adhabu 'nene' ya kutokaa kwenye benchi kwa mechi nne pamoja na faini ya zaidi ya shilingi milioni 30, taarifa ya Chama cha Soka England, (FA) ilisema jana.
Kwa adhabu hiyo, kocha huyo mkali wa kutoa maoni Ligi Kuu England, atatumikia mechi mbili, na kisha mechi zingine mbili anaweza kuongezewa iwapo katika kipindi cha kutumikia adhabu ya mechi mbili za kwanza atafanya kosa lingine.
Lakini kama hatopatikana na kosa lingine, ina maana adhabu yake itakuwa kutumia mechi mbili tu.
Adhabu ya Ferguson imetokana na kauli aliyotoa dhidi ya refa Alan Wiley, aliyemtuhumu kutokuwa na uwezo wa kuchezesha soka wakati alipochezesha mechi kati ya timu yake na Sunderland mwezi uliopita.
Wakati wa kusikiliza shauri lake mjini London, Ferguson, 67, alikiri kutoa kauli hiyo katika mechi iliyomalizika kwa sare ya 2-2 kwenye uwanja wa Old Trafford.
Ferguson alisema Wiley hakuwa na uwezo wa kuchezesha mechi hiyo. Bosi wa tume ya usimamizi, Peter Griffiths, alisema hakuna mashaka kwamba Alex Ferguson alitoa kauli hiyo, ambayo kimsingi hakupaswa kama mwanamichezo.
Alan Leighton, mkuu wa umoja wa marefa, alimtuhumu Ferguson kwa utovu huo wa nidhamu. Ferguson alimponda Wiley wakati wa mahojiano na kituo cha televishen akisema: "Hakuwa kwenye kiwango cha kumchezesha soka."
Ferguson pia aliwahi kutoa maneno yasiyofaa kwa refa Martin Atkinson wakati Manchester United wakifungwa bao 1-0 na Chelsea katika mechi ya Ligi Kuu Jumapili. "Wakati mwingine unakosa imani na refa, ndivyo wanavyosema wachezaji," alisema mara baada ya mechi kumalizika.
Hata hivyo FA, imesema Ferguson hatakumbwa na adhabu kutoka Shirikisho la Soka la Ulimwenguni-FAFA kwa matamshi yake.

No comments:

Post a Comment