Tuesday, November 10, 2009

Liverpool yabanwa mbavu

LONDON, England

KIUNGO Steven Gerrard, jana aliiokoa kipigo Liverpool baada ya kupachika wavuni bao la kusawazisha lililotokana na penati ya utata dhidi ya 'vibonde' Birmingham City, na baada ya dakika 90, matokeo kuwa ya sare ya 2-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya England.
Nahodha Gerrard, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya nyonga, aliingia akitoka benchi la wachezaji wa akiba mwishoni mwa kipindi cha kwanza na kufunga bao la kusawazisha robo ya mwisho ya mchezo.
Penati hiyo ilitolewa baada ya Lee Carsley kumuangusha chini mchezaji wa Liverpool David Ngog, mfungaji wa bao la kwanza."Ni kama utani. Najua kwa ukweli kabisa sikumgusa," alisema Carsley wakati akiongea na ESPN
"Nadhani kama refa (Peter Walton) ataona tukio hili kwenye televisheni, hakika atasikitika sana."
Picha za televisheni zinaonyesha kuwa Carsley, ambaye alipewa kadi ya njano kwa kupinga adhabu hiyo, hakumgusa Ngog.
Liverpool ilionekana kama mambo yangekwenda mazuri baada ya kutangulia kufunga kwa bao la Ngog mapema, lakini mambo yalianza kwenda vibaya dakika ya 26 baada ya Christian Benitez kuisawazishia Birmingham.
Mambo yalikuwa mabaya zaidi baada ya Cameron Jerome kupiga shuti la umbali wa mita 30 na kumshinda kipa wa Liverpool Pepe Reina na kujaa wavuni.
Liverpool, inayoshika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, ilikuwa dimbani bila mshambuliaji wake mahiri Fernando Torres, ilicheza kwa nguvu baada ya mapumziko kujaribu kupata ushindi ili kupunguza pengo la pointi zinazofikia 11 dhidi ya wanaoongoza Chelsea.
Kocha Rafa Benitez ambaye kiti chake kina joto la 'kutimuliwa' kufuatia timu hiyo kufanya vibaya, aliokolewa na penati hiyo ambayo kama isingetinga wavuni, kingekuwa kipigo chake cha sita msimu huu.
"Nimeangalia picha ya televisheni, nadhani haikuwa penati," alisema Benitez wakati akiongea na BBC. "Inawezekana, lakini ukweli ni kwamba tuna wakati mgumu zaidi mwaka huu.
"Tulimiliki mpira kwa kiasi kikubwa na kufanya mashambulizi mengi langoni, lakini hatukuamini kwani mpaka mapumziko tulikuwa nyuma 2-1. Lakini hata hivyo, timu ilionyesha uwezo mkubwa."
Gerrard alicheza, lakini hakuwa fiti kwa asilimia 100. Bado alionyesha kiwango tulichohitaji kukiona," aliongeza Benitez.
Katika mechi hiyo, kiungo Alberto Aquilani alicheza kwa mara ya kwanza tangu ajiungea na klabu hiyo kutoka AS Roma Agosti.
Albert Riera na Yossi Benayoun waliongeza 'donda' la majeruhi Liverpool baada ya kuumia.Birmingham wanabaki katika nafasi ya 15 kati ya timu 20 zinazoshitiki ligi hiyo ikiwa na pointi 12.

No comments:

Post a Comment