Tuesday, November 10, 2009

Yanga yanyoosheana vidole

Na Jacqueline Massano, Jijini

Hali ya mvutano bado inaendelea ndani ya klabu ya Yanga, huku sasa wanachama wakitaka serikali kuingilia kati kuhusu tuhuma za ufujaji wa pesa ndani ya klabu hiyo kongwe nchini, na wakati huo huo wakitaka kuitishwa haraka kwa mkutano mkuu.
Mbali na kutaka kuingilia kati, pia wanataka watuhumiwa wote wa ufisadi wachukuliwe hatua za kisheria.
Baadhi ya wanachama walioongea na blog hii, wameulaumu uongozi kufuatia tuhuma za kupotea zaidi ya shilingi milioni 100 zilizotolewa na wanachama kwa ajili ya kadi.
Mmoja wa wanachama wa klabu hiyo na mchezaji wa zamani, Ramadhan Kampira (003925), alisema sasa imefika hali iliyopo ndani ya klabu ya Yanga haivumilika na serikali ni lazima iingiliea kati ili kunusuru.
Kampira amesema zaidi kuwa, 'utamaduni' wa ubadhilifu wa fedha Yanga sasa ni wa kawaida ndani ya Yanga.
"Kuna watu wachache wanaendelea kunufaika kwa jasho la wengine, nadhani muda umefika waondoke," alisema.
"Hapana sisi kama wanachama tumesema tumechoka, kwani suala la ufujaji wa fedha limekuwa ni tatizo sugu ndani ya klabu yetu. Hawa watafuna pesa za klabu wanaonekana mitaani na magari ya kifahari.
Nadhani mwenyekiti Iman Madega ana kila sababu ya kuitisha mkutano mapema ili kutoa taarifa ya mapato na matumizi tangu uongozi ulipoingia madarakani," aliongeza.
Naye mwanachama mwingine wa klabu hiyo, Omary Hussein ambaye pia aliwahi kuichezea klabu hiyo alisema serikali kupitia Wizara yake ya Michezo ni vyema ikaingilia kati suala la matumizi mabaya ya pesa za klabu ambazo wanachama wamezitoa kwa nia nzuri.
"Huu ni wizi, haiwezekani mtu kula fedha za wanachama kiulani tu, na ndiyo maana klabu yetu imeanza kudidimia kifedha na inashindwa kufanya vizuri, inaumiza sana," alisema.
Hata hivyo, Hussein alimtetea katibu mkuu wa kuajiliwa, Lawrence Mwalusako na kudai kuwa hausiki na tuhuma hizo za ufujaji wa fedha ndani ya klabu hiyo kwa sababu hana muda mrefu tangu aongoze klabu hiyo.
Hata hivyo, Mwalusako alikaririwa akidai kuwa yeye hafahamu chochote kuhusiana na upotevu wa fedha hizo ndani ya klabu hiyo, na kuwataka waandishi wamuulize aliyekuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Lucas Kisasa.

No comments:

Post a Comment