Wednesday, November 18, 2009

Mabao 177 yazamishwa ligi kuu Bara

Na Adam Fungamwango

MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara umemalizika kwa timu zote 12 kucheza mechi 11, huku magoli 177 yakiwa yamepachikwa nyavuni.
Magoli hayo yamefungwa na wachezaji 84 kati ya 323 wanaoshiriki Ligi hiyo kwa michezo 66 ambayo imechezwa, huku magoli 11 yakifungwa kwa mikwaju ya penati.
Pia, takwimu zinaonyesha kuwa raundi ya 11 ambayo ni ya mwisho kwa mzunguko wa kwanza, imevunja rekodi kwa kuwa na magoli mengi kuliko raundi zote za nyuma.
Kabla ya raundi ya 11, raundi ya kwanza ndiyo iliyokuwa na idadi kubwa ya magoli.
Takwimu zinaonyesha kuwa mechi za raundi ya kwanza ambazo zilikuwa za ufunguzi wa Ligi Kuu yalipatikana magoli 19 na idadi hiyo haikuvukwa na raundi zote zilizofuata hadi raundi ya 11 ya kufunga mzunguko wa kwanza ambapo magoli 27 yamepatikana.
Ushindi wa JKT Ruvu wa mabao 4-2 dhidi ya African, Majimaji kuitungua Moro United mabao 3-2, Toto kuitundika Kagera Sugar 2-0, Azam kuisulubu Manyema mabao 4-0, Simba kuitandika Mtibwa Sugar 3-1 na Yanga kuisasambua Prisons mabao 4-2, kumefanya idadi ya magoli kuwa 27 na kuvunja rekodi ya raundi zote.
Kwa upande wa wafungaji, John Bocco wa Azam FC anaendelea kuchanja mbuga ambapo kwa sasa amefikisha magoli tisa na kuzidi kujiwekea mazingira mazuri ya kuwa mfungaji bora mwaka huu.
Hata hivyo anafukuzwa kwa washambuliaji wawili, Hussein Bunu wa JKT Ruvu na Mussa Hassan 'Mgosi' wa Simba ambao wana magoli sita kila mmoja, huku Mrisho Ngassa wa Yanga na Yusuph Soka wa African Lyon wao wakiwa na magoli matano.
Wachezaji Yahaya Tumbo wa Azam, Jerryson Tegete wa Yanga na Yona Ndabila wa Moro United wao wana magoli manne, huku Mbwana Samata wa African Lyon, Danny Mrwanda wa Simba, Michel Katende wa Kagera Sugar, Benedict Ngassa wa Manyema, Maulidi Haniu wa Toto African na Kigi Makasi wa Yanga wakiwa na magoli matatu kila mmoja.

No comments:

Post a Comment