Wednesday, November 18, 2009

Yanga yadaiwa mil. 21

Na Jacqueline Massano

KOCHA msaidizi wa klabu ya mabingwa wa soka nchini-Yanga, Spaso Sokolovisk, ambaye mkataba wake umefikia ukomo katikati ya mwezi huu, anaidai klabu hiyo ya Jangwani shilingi milioni 21.
Kiasi hicho ni malimbikizo ya mishahara ya miezi minne, kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo Alasiri imezipata mapema leo.
"Kwanza ni kweli, Spaso anaidai klabu yetu shilingi milioni 21,440,000 ambazo ni malimbikizo ya mishahara ya miezi minne," alisema mtoa habari ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.
"Hivi sasa viongozi wanaangalia namna ya kupata fedha hizo na kumkabidhi. Tunafahamu mkataba wake umeshakwisha," alisema zaidi.
Akifafanua zaidi, alisema: "Kwa mwezi tulikuwa tunapaswa kumlipa kiasi cha shilingi milioni 5,360,000. Haya ni makubaliano yaliyoko kwenye mkataba."
Bosi wa kitengo cha habari cha klabu hiyo, Louis Sendeu, alikiri kocha huyo kuidai klabu yake, lakini hakuwa tayari kukiri kiasi cha shilingi milioni 21 wanazodaiwa.
"Kweli anatudai, hakuna kificho kwenye hili, tunafanya utaratibu wa kumlipa mapema kama alivyodai," alisema na kuongeza: "Siwezi kusema tunadaiwa kiasi gani, ila kama yeye mwenyewe (Spaso) yuko tayari kusema ni kiasi gani, afanye hivyo."
Bosi Sendeu alimtaka kocha huyo kutulia wakati taratibu za malipo yake zikiandaliwa. "Ninamshauri kuwa mvumilivu, suala lake linajulikana tangu mkataba wake ulipomalizika Nov. 15," aliongeza.
Kutokana na kuchelewa kulipa kwa wakati ,Yanga imejikuta ikiandamwa na madeni mengi, ambapo baada ya mkataba wa kocha wa kwanza, Dusan Kondic kumalizika, klabu hiyo ilijikuta ikidaiwa zaidi ya shilingi milioni 30.

No comments:

Post a Comment