Friday, November 20, 2009

Wachezaji wadundana uwanjani

RIO DE JANEIRO, Brazil

WACHEZAJI wawili wa timu ya Palmeiras Obina na Mauricio wametimuliwa na uongozi wa timu hiyo baada ya kupigana uwanjani, na kisha refa kuwalima kadi nyekundu kwa utovu huo wa nidhamu.
Wawili hao walichapana makonde wakati wakitoka uwanjani kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mapumziko katika mechi waliyofungwa mabao 2-0 na Gremio.
Kwa kosa hilo, Palmeira walilazimika kucheza wakiwa tisa uwanjani kwa kipindi chote cha pili.
"Wachezaji hawa hawatacheza tena soka na Palmeiras," alisema makamu wa rais Gilberto Cipullo wakati akiongea na waandishi wa habari.
Mshambuliaji Obina na mlinzi Mauricio walikuwa wakibishana kufuatia bao la kuongoza la Gremio lililofungwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza na Rafael Marques.
Wakati wanatoka kwa ajili ya kwenda kupumzika kwenye uwanja wa Olimpiki mjini Porto Alegre, ghafla walianza kupigana ngumu kabla ya kutenganishwa na wachezaji wenzao. Lopez alifunga bao la pili kwa Gremio katika dakika ya 70.

No comments:

Post a Comment