Thursday, November 12, 2009

Simba: Yanga karibuni mnuso

Na Adam Fungamwango
WANACHAMA wa Simba tawi la Mburahati kwa Jongo, mwishoni mwa wiki iliyopita walitimiza ahadi yao ya kupika pilau na kula pamoja na wenzao wa Yanga kama sehemu ya furaha ya ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya watani wao wa jadi Oktoba 31 kwenye uwanja wa Taifa.
Mwenyekiti wa Simba tawi la Lion SC la Mburahati kwa Jongo, Abdallah Kipaga, amesema kuwa wameamua kuangusha pilau na kuwakaribisha watani wao baada ya kuwachapa, kutokana na utamaduni waliojiwekea tangu mwaka 2003.
"Sisi Simba tawi la huku na Yanga, tulikaa na kuwekeana utaratibu kuwa timu moja ikishinda, basi wanachama wake watalazimika kuwapikia wenzao pilau ikiwa ni kama njia ya kuwakoga na kuwafariji, hii ilikuwa mwaka 2003 na ndivyo tunavyofanya huku," alisema Mwenyekiti huyo.
Amesema kuwa moja kati ya masharti ambayo wamepeana ni waliofungwa ndiyo wanaokwenda kuchagua mbuzi ambaye atatumika kwenye shughuli hiyo, lakini nao sharti lao ni mwamba wachague mbuzi jike kwa sababu wamefungwa.
"Kwa kweli wikiendi iliyopita tumewalisha Yanga wote wa tawi la Mburahati wa Jongo pilau na utaratibu wetu ni kwamba wao wanakaa tu, sisi kwa sababu tumeshinda ndiyo tunapika, tunawaandalia na tunafanya utani," alisema Kipaga.
Hata hivyo amesema kuwa mwaka jana wenzao hawakuwafanyia hivyo baada ya kuwafunga bao 1-0 na walipowauliza walisema kuwa hali yao ya kiuchumi haikuwa nzuri.
Kipaga amesema kuwa wametumia kiasi cha sh 230,000 kufanikisha hafla hiyo, lakini amesema katika masharti yao timu zikitoka sare hakuna mtu wa kumlisha mwenzake pilau.

No comments:

Post a Comment