Friday, November 27, 2009

Uchaguzi wawagawa mabosi Simba

Na Badru Kimwaga
WAKATI Mhazini Mkuu wa Simba akitangaza dhamira yake ya kujitosa kwenye uchaguzi mkuu wa klabu hiyo, kuna habari kwamba uchaguzi huo huenda usifanyike mwezi ujao kama ilivyotarajiwa na wengi.
Habari za kuaminika zinasema kuwa pamoja na kikao cha Kamati ya Utendaji kukutana Jumapili wiki hii, huenda ikaamuliwa uchaguzi huo kufanyika Januari mwakani.
Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa kumekuwa na mvutano mkubwa juu ya uchaguzi huo ufanyike lini, kundi moja likitaka ufanyike mwezi ujao na jingine kutaka lifanyike mwakani.
"Huwezi kuamini, lakini ukweli ni kuwa viongozi Simba wamegawanyika juu ya lini uchaguzi huo ufanyike, wapo wanaotaka uitishwe mapema na wengine wanapinga wakitoa visingizio muhimu kwa sasa ni ligi kuu," chanzo kilisema.
Habari hizo zinasema kuwa hata kikao cha Jumapili kinaweza kisimalizike vema kama vikao vingine viwili vya klabu hiyo kipindi cha kusaka viongozi wa kuajiriwa kutokana na mgawanyiko huo wa viongozi kuhusu uchaguzi huo.
Hata hivyo Mhazini Mkuu wa Simba, Almas Chano alisema uchaguzi mkuu wao utafahamika rasmi Jumapili baada ya kikao chao cha kamati ya utendaji na kwamba yeye tayari amejipanga kuwania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
"Lini uchaguzi wetu ufanyike, hilo litafahamika baada ya kikao cha Jumapili na sioni watu waanze kuhoji sasa kabla ya kikao hicho," alisema Chano.
Aliongeza kuwa tarehe yoyote utakaofanyika uchaguzi huo, yeye yu tayari kuwania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji na kwamba muda si mrefu ataweka bayana safu yake watakaojipanga kuingia madarakani kuiongoza Simba.
Viongozi wa sasa Simba waliingia madarakani Desemba 3, 2006, nao ni Hassani Dalali, Omar Gumbo, Mwina Kaduguda, Mohammed Mjenga, Idd Senkondo, Almas Chano na Said 'Seydou' Rubeya.

No comments:

Post a Comment