Friday, November 27, 2009

Yanga yaongoza kwa kesi TFF

Na Jacqueline Massano, Jijini
MSHAMBULIAJI wa kimataifa, Boniface Ambani amesema ataichongea klabu Yanga ya jijini Dar es Salaam iliyotangaza kumwaga mwanzoni mwa wiki hii, Shirikisho la Soka nchini TFF iwapo klabu hiyo itashindwa kumlipa madai yake kwa wakati.
Ambani raia wa Kenya ambaye amecheza Yanga misimu miwili, anaidai klabu hiyo kufuatia kuvunjwa kwa mkataba wake miezi sita kabla.
Akiongea na blog hii mapema leo, Ambani alisema anatarajia kuwasili nchini, Jumatatu kwa ajili ya kufatilia madai yake kabla ya kwenda Ethiopia alipoitwa na kocha wa zamani wa klabu hiyo, Milutin Sredejovic 'Micho'.
"Safari yangu ya kuja Dar ni pamoja na kufuatilia pesa zangu Yanga baada ya kuvunjwa kwa mkataba. Ni vyema Yanga wakaharakisha kunilipa madai yangu," alisema.
Iwapo Ambani atakwenda kuishitaki Yanga TFF, atakuwa mchezaji wa pili katika kipindi kifupi baada ya mchezaji mwingine aliyetemwa katikati ya msimu, beki Hamis Yusuf kwenda kuishitaki klabu hiyo kwa kile kinachodaiwa kuvunjwa kwa mkataba wake.
Msimu iliopita, Yanga ilikutana tena na mashitaka TFF baada ya mchezaji wake raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Aime Lukunku kuishitaka baada ya kutelekezwa kwa muda mrefu bila kulipwa madai yake.
Mbali na wachezaji hao, pia kocha aliyemaliza mkataba wake, Dusan Kondic aliwahi kuishitaki klabu hiyo TFF baada ya kuchelewa kumlipa mshahara wake wa miezi minne zaidi ya shilingi milioni 30.
Kocha mwingine anayeidai klabu hiyo na ambaye anaweza kupiga hodi TFF kushinikiza kulipwa madai yake ni aliyekuwa msaidizi wa Kondic, Spaso Solokovisk ambaye anaidai klabu zaidi ya shilingi miluioni 21.

No comments:

Post a Comment