Monday, November 23, 2009

Yanga yamchanganya Micho

Na Jacqueline Massano

BAADA ya uongozi wa klabu ya Yanga ya Jijini kutangaza kuwaacha wachezaji watano akiwemo mshambuliaji mkenya Boniface Ambani, aliyewahi kocha mkuu wa timu hiyo, Milutin Sredejovic 'Micho' amesikitishwa na hatua hiyo.
Akizungumza na Alasiri kwa njia ya simu jana, Micho huyo ambaye kwa sasa anaifundisha timu ya St. George ya Ethiopia amesema Yanga kwa kuwatema wachezaji hao imepotea njia.
Wiki iliyopita, klabu hiyo bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara imetangaza kuwatema wachezaji watano akiwemo Ambani, Joseph Shikokoti, George Owino, Yusuf Hamis na Vincent Barnabas ambaye amewekwa 'bondi' African Lyon.
"Hawa Yanga, naona wameanza kuishiwa kwa nini wameawaacha wachezaji hao wakati ni wazuri... ni nini kimewasibu," alihoji kocha huyo wakati akizungumza na Alasiri.
Kocha huyo alisema kama Yanga imeamua kuwaacha wachezaji kwa sababu ya kushuka kiwango chao."Hivi ni kweli wachezaji hawa kiwango chao kimeshuka, au hawana nidhamu, nataka nijue kwa undani zaidi. Kwanini wameachwa, mimi sijui ila kwa sababu ya kiwango, sina hakika.
"Na kama inawezekana naomba nipe namba ya Ambani ili nizungumze naye nipate jinsi ya kumsaidia, tafadhali fanya hivyo," aliongeza kocha huyo.
Hata hivyo, Alasiri ilipozungumza na Ambani kutaka kufahamu kama amewasiliana na kocha huyo alisema: "Bado hatujawasiliana."
Ambani alisema kwa sasa ameanza taratibu za kutafuta timu nje ya nchi na muonekano unaonyesha mafanikio katika zoezi hilo.
"Kama Yanga wameniacha sijali, kwa sababu nimeanza taratibu za kutafuta timu nje yaBongo," alisema Ambani.

No comments:

Post a Comment