Thursday, December 3, 2009

Arsenal, Chelsea nje Kombe la Ligi

Man U, Man City nusu fainali
London, England

MAJIRANI Manchester City na Manchester United, watakumbana katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Ligi, huku Blackburn Rovers wakikutana na Aston Villa katika hatua hiyo hiyo.
Blackburn Rovers ilipata ushindi jana baada ya kuwaangusha vinara wa Ligi Kuu England, Chelsea iliyokuwa na wachezaji 10 dimbani kwa penati 4-3 baada ya kumaliza dakika 120 kwa sare ya mabao 3-3 kwenye uwanja wa Ewood Park.
Chelsea walijikuta wakiwa nyuma mara mbili kabla ya kusawazisha bao katika dakika ya 122 na kupelekea mchezo kuamuliwa kwa njia ya mikwaju ya penati.
Matajiri wa Manchester, Manchester City 'waliwaonea' chipukizi wa Arsenal kwa kuwatandika mabao 3-0 katika mechi nyingine ya robo, matokeo ambayo sasa yatawakutanisha na majirani zao Manchester United katika hatua ya nusu fainali.
Ikicheza bila kocha wao, Sam Allardyce ambaye amefanyiwa upasuaji wa moyo, Blackburn ilikuwa ya kwanza kutikisa nyavu za Chelsea kupitia kwa mshambuliaji wa Croatia, Nikola Kalinic dakika tisa tangu kuanza kwa mchezo.
Kocha wa Chelsea, Carlo Ancelotti alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu kwa wakati mmoja, na dakika tatu baadaye mshambuliaji Didier Drogba aitumbukiza mpira wavuni, na kisha Salomon Kalou kufunga bao lingine na kuifanya Chelsea kuwa mbele kwa mabao 2-1, lakini Blackburn walisawazisha baada ya kipa Hilario kushindwa kucheza mpira wa krosi uliopigwa na Brett Emerton.
Kalou aliumia katika dakika ya 73 na kulazimika kutoka nje na hivyo Chelsea kubaki na wachezaji 10 uwanjani.
Blackburn walikwenda mbele na kufunga bao ndani ya muda wa nyongeza kupitia kwa mshambuliaji Benni McCarthy, lakini bao la Paulo Ferreira wa Chelsea lilifanya matokeo ya mwisho kuwa 3-3.
Kalinic na Michael Ballack wa Chelsea walikosa penati, kabla ya Robinson kuokoa mpira wa penati dhaifu ya Kakuta.

No comments:

Post a Comment