Friday, December 4, 2009

Bingwa 'World Cup' kulamba bil. 30

Afrika Kusini
BINGWA wa fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, atajinyakulia donge nono--dola mil. 30 (zaidi ya bil. 30), taarifa ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA lilisema jana kufuatia mkutano wake uliofanyika kwenye kisiwa cha Robin.
Aidha, mshindi wa pili atajinyakulia dola mil. 24 (sawa na bil. 24), huku kila timu itakayoshiriki ikipata bilioni 1 kama gharama ya maandalizi kwa ajili ya fainali hizo, taarifa zaidi ilisema.
Maamuzi hayo yalifikiwa jana katika kikao cha Kamati ya Utendaji cha FIFA kilichofanyika kwenye kisiwa cha Robben, nchini Afrika Kusini ambapo Nelson Mandela alishikiliwa kwa muda wa miaka 18 na utawala wa wazungu wakati huo.
Rais wa FIFA, Sepp Blatter na katibu mkuu wa Shirikisho hilo, Jerome Valcke walikuwa wakiongea na waandishi wa habari 250 waliosafiri na boti kutoka mji wa Cape Town kwenda kisiwa cha Robben.
Valcke alisema kuwa jumla ya zawadi zote kwa timu 32 ni shilingi bilioni 420, ikiwa ni ongezeko la asilimia 61 kutoka shilingi bilioni 261.4 kwenye fainali zilizofanyika nchini Ujerumani mwaka 2006.
Watakaofikia hatua ya nusu fainali watapata shilingi bilioni 20, wakati timu zitakazogusa hatua ya robo fainali zitanyakua bilioni 18, huku timu zitakazofikia raundi ya pili zitaondoka na bilioni 9, na zile zitakazotolewa kwenye hatua ya makundi kila mmoja ataondoka na bilioni 8.
Vile vile, Valcke alisema kuwa FIFA itatoa kiasi cha shilingi bilioni 40 kwa timu ambazo wachezaji wake watashiriki kwenye michuano hiyo.
"Kila klabu ambayo itakuwa na mchezaji kwenye fainali hizo, itapata kiasi cha milioni 1.8 kwa siku," alisema Valcke. "Pesa hizo zitalipwa siku 15 kabla ya kuanza kwa michuano, na siku moja baada ya wachezaji kuanza kucheza kwenye fainali hizo.
"Pesa ambazo zitalipwa klabu zitapitia kwenye vyama vya soka, huku pia vilabu vikikubali kutochukua hatua yoyote ya kudai fidia kupitia mahakama za madai, lakini kama ipo sababu, basi vitafanya hivyo kupitia FIFA, au CAS--mahakama ya kimataifa ya Michezo.

No comments:

Post a Comment