Friday, December 4, 2009

Wambura aishukia Simba

Na Daniel Mkate

HUKU akiendelea kupigwa 'danadana' kuhusu kadi mpya ya uanachama wa klabu ya Simba, Michael Wambura, ameutaka uongozi wa klabu hiyo umuuleze tatizo alilonalo kiasi cha kutopewa kadi yake.
Wambura alisema hajafahamu kosa alilofanya hata kusababisha kuzungushwa kukabidhiwa kadi yake.
"Sielewi huu uongozi unanigwaya nini, sijatangaza kuwania uongozi, ninachotaka ni kadi yangu tu ambayo ni mali yangu halali...sidaiwi, nimelipia ada zote za uanachama," alisema Wambura.
Alisema mpaka sasa anazungushwa kama 'daladala', kwani akienda kwa mhasibu wa klabu hiyo, Chano Almasi, anaambiwa aende kwa mwenyekiti Hassan Dalali ambaye 'humkimbia'.
"Dalali nikimpigia simu anakata na kisha kuzima kabisa, sasa sielewi nina tatizo gani kwa uongozi huo kwani kadi ni mali yangu wala haitakiwi kukalishwa vikao ili nipewe," alisema.
Aidha, Wambura alisema kadi hiyo yenye namba 2704, inaonekana anafanyiwa 'kauzibe' asipewe kwa lengo la kuwafurahisha watu fulani.
Wambura alisema iwapo viongozi hao wanadhani kukabidhiwa kadi hiyo kutamfanya awanie moja ya nafasi katika klabu hiyo, basi anawaomba wasiwe waoga wa uchaguzi.

No comments:

Post a Comment