Tuesday, December 29, 2009

Kipigo kingine chaisubiri Simba

*Yanga yatamba
Na Jacqueline Massano

KATIKA mwendelezo wa kunogewa na furaha ya ushindi dhidi ya watani wao wa jadi Simba, mabingwa wa soka nchini, Yanga imesema ingetamani kupata nafasi nyingine ya 'kuionea' Simba wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajia kuanza baadaye mwezi ujao Visiwani, Zanzibar.
Yanga ilimaliza uchovu wa kutoondoka na furaha kila inapokutana na Simba baada ya kuwanyuka Wekundu hao wa Msimbazi mabao 2-1 katika mechi ya dakika 120--nusu fainali ya michuano ya Kombe la Tusker iliyomalizika kwa Yanga kutwaa ubingwa.
Simba, mabingwa wa soka nchini, Yanga na Mtibwa zitashiriki kutoka Bara, wakati wenyeji timu za Kisiwani Zenji ni pamoja na Malindi, Miembeni, Jamhuri, Zanzibar Ocean View na Mafunzo.
Afisa Uhusiano wa Yanga, Louis Sendeu amesema kuwa kikosi chako kwa sasa kiko imara kukabiliana na timu yoyote, na italeta furaha kama watakutana tena na Simba kwenye michuano hiyo.
Katika michuano ya Tusker, Simba ilimaliza kwa kushika nafasi ya tatu, kufuatia ushindi wa jasho jingi lililokauka baada ya dakika 120 na kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tusker ya Kenya katika mechi ya nusu fainali, huku Tusker ikikosa nafasi hiyo kiduchu baada ya kuwa mbele bao 1-0 mpaka dakika za majeruhi kabla ya Simba kusawazisha na kupelekea nyongeza ya dakika.
Alisema kuwa ushindi mafanikio mazuri waliyopatra kwenye michuano ya Tusker imefungua njia zaidi ya ushindani hasa katika michuano ya Ligi Kuu.
"Kama tutapangwa kundi moja na Simba, au ikatokea kukutana katika hatua yoyote, basi hii ndiyo furaha yetu. Kwa sasa tunaweza kuifunga Simba tunavyotaka. Ilikuwa makosa kudhani kwamba Simba haifungiki," alisema.
Wakati Yanga wakikosa mapumziko baada ya michuano ya Tusker, wapinzani wao Simba wako mapumzikoni mpaka Januari 2. Kwa mujibu wa Sendeu, timu yao inaanza mazoezi leo kwenye uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika, IST.
Hata hivyo taarifa za hofu kwamba Simba huenda isishiriki michuano hiyo, zimezimwa leo baada ya kuthibitisha ushiriki wao kupitia mtoa habari Clifford Ndimbo.
Ndimbo amesema kuwa, klabu yao itashiriki michuano hiyo kama ilivyopangwa, na kwamba wanatarajia kuanza mazoezi muda mfupi baada ya kurejea kocha Patrick Phiri aliyerudi zambia kwa mapumziko mafupi.

No comments:

Post a Comment