Monday, December 28, 2009

Simba wamgeuzia kibao Phiri

BAADA ya kuchapwa mabao 2-1na mahasimu wao Yanga katika mechi ya nusu fainali ya kombe la Tusker, Simba sasa wameamua kumgeuzia kibao kocha wao mkuu, Mzambia Patrick Phiri.
Baadhi ya mashabiki, wapenzi na manazi wa timu hiyo wamesema kocha huyo ndiyo sababu kubwa ya kufungwa na Yanga, na kisha wachezaji kucheza chini ya kiwango katika michuano hiyo iliyomalizika kwa klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani kutwaa taji.
Wakizungumza baada ya pambano lao la Alhamisi kumalizika, wapenzi hao wa Simba wakasema kitendo cha Phiri kuondoka na kwenda mapumzikoni nyumbani kwao Zambia na kuwapa mapumziko ya muda mrefu wachezaji, ndiyo sababu iliyosababisha wachezaji hao kuporomoka viwango.
"Kama kocha angekuwepo kambini na timu huko Zanzibar na kutoa mazoezi kama yale anayowapa katika Ligi Kuu Bara, basi wana imani wasingefungwa na kunyanyaswa na Yanga uwanjani na pia kuchukua ubingwa," alisema Muhidin Parojo mnazi wa Simba.
Simba timu inayochukuliwa kama ni kioo cha michuano hiyo, imecheza katika kiwango duni na kuwashangaza mashabiki waliozoea kuiona ikicheza Ligi Kuu mechi 11 bila kufungwa wala kutoka sare."
Katika mechi ua kusaka mshindi wa tatu, Simba waliishinda Tusker kwa mabao 2-1 na kushika nafasi ya tatu.Mashabiki wengi wamemtaka kocha Phiri kutowapa mapumziko tena wachezaji wake na badala yake awafanyishe mazoezi makali mara baada ya mwaka mpya kuanza.

No comments:

Post a Comment