Monday, December 28, 2009

Yanga yaitisha Simba

UONGOZI wa klabu ya Simba umekiri mahasimu wao Yanga walistahili kutwaa ubingwa wa michuano ya kombe la Tusker kutokana na kujiandaa vizuri kuliko wao.
Aidha, uongozi huo umewataka wanachama wao kuacha kumsaka mchawi kwa matokeo yaliyowatokea katika michuano hiyo iliyomalizika jana, na badala yake kutakiwa kushikamana kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu nchini.
Katibu Msaidizi wa klabu hiyo, Mohammed Mjenga, alisema watani wao walionekana kubadilika kisoka kwa kucheza mpira wa pasi na kwa kiwango hicho walistahili kuwa mabingwa wa Tusker.
Mjenga alisema ni dhahiri Yanga walijiandaa vyema kwa michuano hiyo tofauti na Simba na ndio maana waliweza kuibuka washindi katika mechi yao na hawana la kusingizia zaidi ya kuridhika na matokeo.
Alisema hata hivyo pamoja na kuwapa heko watani zao, bado binafsi anawatupia lawama waamuzi kwa kuonyesha udhaifu katika michuano hiyo."Tatizo la waamuzi ni sugu na hatujui litaisha lini, ni kama hawajui wajibu wao wawapo uwanjani," alisema Mjenga.
Pia aliwataka wanachama wa Simba kuacha kumsaka mchawi kutokana na matokeo ya mechi yao na Yanga na badala yake kushikamana pamoja kwa ajili ya kujiandaa na duru la pili la ligi kuu pamoja na Kombe la Shirikisho.
Mjenga alisema, lawama kwa sasa wakati muafaka, ila umoja na mshikamano pamoja na kumsapoti kocha na wachezaji kwa michuano iliyopo mbele yao ndio kitu cha muhimu zaidi.

No comments:

Post a Comment