Monday, November 30, 2009

KIPA MPYA YANGA KUJARIBIWA LEO

WAKATI ikiendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kipa mpya wa Yanga kutoka Ghana, Yaw Berka anatarajiwa kufanyiwa majaribio leo uwanjani hapo.
Berka ambaye aliwahi kuichezea timu ya tifa ya vijana ya Ghana, atafanyiwa majaribio akiwa chini ya kocha mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic.
Yanga kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kusajili wachezaji katika dirisha dogo la usajili ambalo linafikia tamati leo.

PICHA YA WIKI


UCHAGUZI SIMBA MWAKANI

WAKATI wanachama wa klabu ya Simba wakilicharukia Shirikisho la Soka nchini, TFF, kuwa limekwamisha kufanyika kwa uchaguzi mkuu, uongozi wa klabu hiyo umetangaza uchaguzi huo sasa utafanyika Januari 17, mwakani.
Kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo iliyokutana usiku wa kuamkia leo, umeamua kwa kauli moja kuwa uchaguzi huo utafanyika Januari mwakani na wala si Desemba mwaka huu kama ilivyokuwa ikitarajiwa na wengi.
Kwa mujibu wa taarifa toka kwa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ni kwamba kikao hicho kimeamua uchaguzi huo kufanyika tarehe hiyo ili kupisha zoezi la ugawaji wa kadi, kikao cha mapato na matumuzi na mkutano mkuu.

Sunday, November 29, 2009

Ibrahimovic aipa ushindi Barca

ZLATAN Ibrahimovic aliingia uwanjani akitokea katika benchi la wachezaji wa akiba na kuipatia Barcelona ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao wakubwa Real Madrid na kuirejesha timu hiyo kileleni mwa msimamo wa La Liga.
Mshambuliaji wa Sweden Zlatan Ibrahimovic alifunga bao pekee lililoitoa Barcelona kifua mbele baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Real Madrid nyumbani na kurejea kileleni mwa msimamo wa Primera Liga.\Mchezaji huyo alifunga bao hilo katika dakika ya 56 na Barca ilijikuta ikipata pigo baada ya mchezaji wake Sergio Busquets kutolewa nje kwa kadi nyekundu muda mfupi baada ya bao hilo, lililoiwezesha timu hiyo kuwa pointi mbili zaidi kileleni dhidi ya wapinzani wake hao wakubwa ikiwa na pointi 30 baada ya kucheza mechi 12.

CHELSEA YAICHAMBUA ARSENAL

LONDON, England
Chelsea bado imeendelea kuongoza kwa pointi tano kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England na kupunguza makali ya baadhi ya timu zinazoifukuza katika kinyang'anyiro hicho baada ya kuibuka na ushindi wa bao 3-0 ugenini kwenye uwanja wa Emirates na kuiacha Arsenal ikiwa nyuma kwa pointi 11.

Friday, November 27, 2009

Yanga yaongoza kwa kesi TFF

Na Jacqueline Massano, Jijini
MSHAMBULIAJI wa kimataifa, Boniface Ambani amesema ataichongea klabu Yanga ya jijini Dar es Salaam iliyotangaza kumwaga mwanzoni mwa wiki hii, Shirikisho la Soka nchini TFF iwapo klabu hiyo itashindwa kumlipa madai yake kwa wakati.
Ambani raia wa Kenya ambaye amecheza Yanga misimu miwili, anaidai klabu hiyo kufuatia kuvunjwa kwa mkataba wake miezi sita kabla.
Akiongea na blog hii mapema leo, Ambani alisema anatarajia kuwasili nchini, Jumatatu kwa ajili ya kufatilia madai yake kabla ya kwenda Ethiopia alipoitwa na kocha wa zamani wa klabu hiyo, Milutin Sredejovic 'Micho'.
"Safari yangu ya kuja Dar ni pamoja na kufuatilia pesa zangu Yanga baada ya kuvunjwa kwa mkataba. Ni vyema Yanga wakaharakisha kunilipa madai yangu," alisema.
Iwapo Ambani atakwenda kuishitaki Yanga TFF, atakuwa mchezaji wa pili katika kipindi kifupi baada ya mchezaji mwingine aliyetemwa katikati ya msimu, beki Hamis Yusuf kwenda kuishitaki klabu hiyo kwa kile kinachodaiwa kuvunjwa kwa mkataba wake.
Msimu iliopita, Yanga ilikutana tena na mashitaka TFF baada ya mchezaji wake raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Aime Lukunku kuishitaka baada ya kutelekezwa kwa muda mrefu bila kulipwa madai yake.
Mbali na wachezaji hao, pia kocha aliyemaliza mkataba wake, Dusan Kondic aliwahi kuishitaki klabu hiyo TFF baada ya kuchelewa kumlipa mshahara wake wa miezi minne zaidi ya shilingi milioni 30.
Kocha mwingine anayeidai klabu hiyo na ambaye anaweza kupiga hodi TFF kushinikiza kulipwa madai yake ni aliyekuwa msaidizi wa Kondic, Spaso Solokovisk ambaye anaidai klabu zaidi ya shilingi miluioni 21.

Uchaguzi wawagawa mabosi Simba

Na Badru Kimwaga
WAKATI Mhazini Mkuu wa Simba akitangaza dhamira yake ya kujitosa kwenye uchaguzi mkuu wa klabu hiyo, kuna habari kwamba uchaguzi huo huenda usifanyike mwezi ujao kama ilivyotarajiwa na wengi.
Habari za kuaminika zinasema kuwa pamoja na kikao cha Kamati ya Utendaji kukutana Jumapili wiki hii, huenda ikaamuliwa uchaguzi huo kufanyika Januari mwakani.
Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa kumekuwa na mvutano mkubwa juu ya uchaguzi huo ufanyike lini, kundi moja likitaka ufanyike mwezi ujao na jingine kutaka lifanyike mwakani.
"Huwezi kuamini, lakini ukweli ni kuwa viongozi Simba wamegawanyika juu ya lini uchaguzi huo ufanyike, wapo wanaotaka uitishwe mapema na wengine wanapinga wakitoa visingizio muhimu kwa sasa ni ligi kuu," chanzo kilisema.
Habari hizo zinasema kuwa hata kikao cha Jumapili kinaweza kisimalizike vema kama vikao vingine viwili vya klabu hiyo kipindi cha kusaka viongozi wa kuajiriwa kutokana na mgawanyiko huo wa viongozi kuhusu uchaguzi huo.
Hata hivyo Mhazini Mkuu wa Simba, Almas Chano alisema uchaguzi mkuu wao utafahamika rasmi Jumapili baada ya kikao chao cha kamati ya utendaji na kwamba yeye tayari amejipanga kuwania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
"Lini uchaguzi wetu ufanyike, hilo litafahamika baada ya kikao cha Jumapili na sioni watu waanze kuhoji sasa kabla ya kikao hicho," alisema Chano.
Aliongeza kuwa tarehe yoyote utakaofanyika uchaguzi huo, yeye yu tayari kuwania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji na kwamba muda si mrefu ataweka bayana safu yake watakaojipanga kuingia madarakani kuiongoza Simba.
Viongozi wa sasa Simba waliingia madarakani Desemba 3, 2006, nao ni Hassani Dalali, Omar Gumbo, Mwina Kaduguda, Mohammed Mjenga, Idd Senkondo, Almas Chano na Said 'Seydou' Rubeya.

Grant kocha mpya Portsmouth

LONDON, England
Avram Grant ametangazwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Portsmouth akichkua nafasi ya kocha Paul Hart aliyetimuliwa mwanzoni mwa wiki hii, taarifa ya klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya England ilisema jana.
"Avram ni kocha mwenye uzoefu na anaheshimika kwa kiwango chake cha juu ufundishaji. Bodi ya wakurugenzi inaamini kuwa ataisaidia klabu kuepuka kushuka daraja," alisema mwenyekiti mtendaji Peter Storrie kupitia tovuti ya klabu hiyo.
Grant atakuwa kwenye benchi la timu hiyo Jumamosi wiki hii wakati atakapopambana na Manchester United.
"Anaijua klabu, wachezaji na mfumo mzima hapa Fratton Park, hivyo ni sahihi kumtangaza kuwa kocha," alisema Storrie.

Sissoko akerwa na Ubaguzi wa rangi

MILAN, Italia
KIUNGO wa Juventus, Mohamed Sissoko amezitaka mamlaka zinazosimamia mchezo wa soka kuchukua hatua kali zaidi baada ya mashabiki wa klabu hiyo kuonyesha vitendo vya ubaguzi wa rangi.
Juve ililazimika kucheza bila watazamaji wake msimu uliopita kufuatia mashabiki wake kuimba nyimbo za ubaguzi wa rangi wakimlenga mchezaji wa Inter Milan, Mario Balotelli waliposema, 'hakuna mtaliano mweusi'.
Klabu hiyo ilitozwa faini kufuatia kuendelea kutoa maneno ya kibaguzi dhidi ya mchezaji huyo mwenye asili ya Afrika kwenye mechi ya Jumapili waliyoshinda bao 1-0.
Hata hivyo, vitendo hivyo vilishuhudiwa tena kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa waliyofungwa bao 1-0 dhidi ya Bordeaux Jumatano wiki hii
Sisi kama wachezaji tunapinga vitendo hivi," alisema Sissoko mchezaji wa kimataifa wa Mali wakati akiongea na Radio ya Italia Alhamisi."
Juventus imechukua hatua zote kuhakikisha vitendo hivi havitokei tena, lakini ni jukumu la mamlaka zingine kuingilia kati.
"Shirikisho la Soka Ulaya-UEFA litafanya uchunguzi kuhusu madai hayo ambayo yanaweza yasiwe na nguvu kwa vile yalitokea kabla ya kuanza kwa mchezo hivyo kutokuwepo kwenye ripoti ya mwamuzi.
Juventus wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo, wanatarajia kupambana na vinara wa ligi hiyo Inter Milan Dec. 5, na kocha Jose Mourinho amesema ingekuwa jambo zuri kama mchezo huo ungehamishwa toka Turin.

Haya sasa!

Thursday, November 26, 2009

Jamani, mnamjua huyu demu? Toeni maoni yenu!



Jamani kaka! Aah, hata sikuwezi!

Mhariri wa Michezo wa gazeti la Alasiri, Joseph Kapinga 'Kaps' (kushoto) akiwa na mwanamuzi wa Benin, Angelique Kidjo wakati alipotembelea Buza, Dar es Salaam.

Wagombea Simba wapigwa mkwara

Na Badru Kimwaga
BAADHI ya wanachama wa klabu ya soka ya Simba wamewataka viongozi wa sasa wa klabu hiyo wenye dhamira ya kurejea tena madarakani wajitokeze kugombea, lakini wawe na majibu ya ahadi zao walizoshindwa kuzitekeleza.
Wanachama hao walisema kuwa kabla viongozi hao hawajawaomba kura siku ya uchaguzi huo ni lazima waambie zile ahadi zao walizotoa mwaka 2006 ziliishia wapi na kuwaridhisha ili wawapigie tena kura kurejea uongozini.
Mmoja wa wanachama waliotoa 'mkwara' huo ni Zubeir Mpacha mwenye kadi namba 297, aliyesema viongozi wao wa sasa walitoa ahadi kemkem ambazo hakuna iliyotekelezwa na hivyo wanataka kwanza majibu yake.
Mpacha alisema viongozi hao waliahidi kujenga kisima, kuifanya Simba kama Zamalek, kulikarabati jengo na nyingine ambazo hakuna hata moja iliyotekelezwa, hivyo watakaowania tena uongozi wawaje majibu wawape kura.
"Tumesikia wakitangaza kuja kuwania tena uongozi, tunawakaribisha, lakini tunataka kabla ya kutuomba kura watueleze ahadi zao ziliishia wapi kama hawana majibu ni bora watulie makwao," alisema Mpacha.
Mwanachama mwingine, Issa Said Ruchaki 'Masharubu' (2511) alisema kwa vile katiba inawaruhusu viongozi hao kuomba tena, wajitokeze ila wafanye kazi ya ziada kuwashawishi wanachama kupata kura zao uchaguzi huo ujao.
Pia aliutaka uongozi huo kabla ya kuitisha uchaguzi huo uitishe mkutano wa wanachama ili ijulikane watafanya uchaguzi huo kwa katiba ipi kwa kuhofi kuna uwezekano Simba ikaingia kwenye mgogoro wa kikatiba baadae.
Viongozi wa sasa walitangaza dhamira ya kuwania uongozi katika uchaguzi huo ujao ni Mwenyekiti Hassan Dalali na Makamu wake, Omar Gumbo, huku wanachama wengine Ismail Aden Rage na Bossy Matola nao 'wamejitosa' pia.
Uchaguzi huo wa Simba unatarajiwa kutangazwa rasmi Jumamosi ijayo baada ya kufanyika kwa kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo, ambacho hata hivyo zipo habari kuwa kimeahirishwa.

Man Utd, Juventus chali

LONDON, England
BAYERN Munich, juzi ilijiweka katika nafasi nzuri ya kujinasua katika hatari ya kutolewa mapema katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kuichapa Maccabi Haifa bao 1-0, huku wapinzani wao Juventus wakipokea kipigo kutoka kwa Girondins Bordeaux.
AC Milan wenyewe walikosa nafasi ya kujihakikishia kucheza hatua ya timu 16-bora baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Olympique Marseille, wakati Real Madrid ilipiga hatua moja mbele kuisogelea raundi ya pili kwa kuifunga FC Zurich 1-0 katika mechi ambayo winga Cristiano Ronaldo alikuwa dimbani baada ya muda mrefu wa kuwa majeruhi.
Manchester United, ambayo tayari ilishafuzu kwa raundi ya pili, ilijikuta ikiharibu rekodi yake ya kutofungwa mechi 23 nyumbani katika mashindano hayo baada ya kufungwa 1-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Old Trafford na timu ya Uturuki ya Besiktas.
Matokeo ya mechi za juzi hajaongeza idadi ya timu ambazo tayari zilizofuzu kwa hatua ya timu 16-bora, Girondins Bordeaux, Olympique Lyon, Arsenal, Manchester United, Chelsea, Porto, Fiorentina na Sevilla -- nafasi nane zilizobaki zitajazwa katika mechi za mwisho zitakazochezwa mwezi ujao.
Hatahivyo, bahati mbaya ya Bayern haikuwa mikononi mwao wakati mchezo huo ukianza, ambapo ilijua wazi kuwa ushindi kwa Juventus dhidi ya timu ambayo tayari ilishafuzu ya Bordeaux ungeiwezesha timu hiyo ya Italia kufuzu kwa raundi inayofuata.
Ikikabiliana na timu ambayo haijapata pointi hata moja au bao, Bayern ilifanya vitu vyake wakati Mcroatia Ivica Olic alipoipatia timu hiyo bao la ushindi katika dakika ya 62 alilofunga baada ya kuuwahi mpira uliorudi uwanjani na kuiwezesha timu hiyo kupata bao la kwanza nyumbani katika mechi tatu walizocheza katika kundi laoTimu ya Bordeaux inayofundishwa na Louis van Gaal iliibuka na ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Juventus huku mabao yakifungwa na Mbrazil Fernando na Mmorocco Marouane Chamakh katika kipindi cha pili.

Jinsi nyasi zilivyochimbika jana, ligi ya Mabingwa Ulaya

Ji-Sung Park (katikati) wa Manchester United akichuana na mchezaji wa Besiktas, Fabian Ernst (kushoto) na Ibrahim Toraman wakati wa mechi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa mjini Manchester, jana.
Mchezaji wa Chelsea, Drogba (kulia) akiwatoka Alvaro Pereira na Raul Meireles (nyuma) wa Porto katika mechi ya Ligi ya Mabingwa mjini Porto jana.

Diego Forlan (kulia) wa Atletico Madrid akiwania mpira na mchezaji wa APOEL Nicosia, Savvas Poursaitides katika mechi ya Ligi ya Mabingwa kwenye dimba la GSP mjini Nicosia jana.

Mchezaji wa Real Madrid, Kaka akikimbia na mpira huku mchezaji wa FC Zurich, Alain Rochat wakati wa michuano ya Ligi ya Mabingwa mjini Madrid jana.
Pato wa AC Milan (katikati) akichuana na wachezaji wa Olympique Marseille, Edouard Cisse (kulia) na Gabriel Heinze wakati mechi ya Ligi ya Mabingwa huko San Siro mjini Milan jana. Picha zote na REUTERS

Obama na my wife wake walivyopendeza

Wednesday, November 25, 2009

Ambani kujaribiwa St. George

Na Jacqueline Massano

MSHAMBULIAJI Mkenya aliyetemwa Yanga katika usajili wa dirisha dogo, Boniface Ambani, ameitwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mserbia Milutin Sredejovic 'Micho' ambaye kwa sasa anaifundisha St. George ya Ethiopia kwa ajili ya kufanya majaribio.
Ambani ametemwa na klabu hiyo kwa madai ya kushuka kiwango na kushindwa kumshawishi kocha mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic.
Akizungumza na blog hii kwa njia ya mtandao, Micho alisema tayari amefanya mazungumzo na mchezaji huyo ili aweze kufanya majaribio kwenye timu yake.
"Ngoja aje nimuone maana siwezi kuzungumza na mtu bila hata kujua kiwango chake, akija hapa nitamfanyia majaribio na kuangalia kiwango chake na akinifurahisha nitamsajili kwa kipindi hiki," alisema Micho.
Micho alisema ikiwa kiwango cha mchezaji huyo hakitamridhisha basi atamuacha ili aweze kutafuta timu nyingine ya kuichezea.
"Huku St. George kwanza kabisa tunazingatia nidhamu na bidii ya mchezaji akiwa uwanjani, na kiwango chake kikiwa hakifurahishi tunaachana naye," alisema.
Hata hivyo, Alasiri ilipowasiliana na Ambani kutoka Kenya, alikiri kufanya mazungumzo na kocha huyo na kudai kwa sasa anasubiri kuitwa.
"Nilikuwa na safari ya kwenda kufanya majaribio kwenye timu nyingine, lakini mara baada ya kupokea simu ya Micho ikinihitaji kwenda Ethiopia, nimesitisha mishemishe zangu, na sasa nasubiri mipango ya kuondoka kwangu," alisema Ambani.
Ambani mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu ijayo kwa ajili ya kufuatilia malipo yake ya kuvunjiwa mkataba na klabu yake ya zamani, Yanga.

Man United, Chelsea kibaruani leo

MILAN, Italia

TIMU mbili za Uingereza, Manchester United 'Red Devils' na Chelsea 'The Blues' ambazo tayari zimefuzu hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, leo zina kazi nyepesi zikiwa zinaelekea ukingoni mwa mechi za hatua ya makundi pale zitakaposhuka katika viwanja tofauti.
Man United itakuwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford itakapoikaribisha Besiktas katika mechi ya kundi B ya michuano hiyo.
Wakati mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Uingereza wakiwa uwanja wa nyumbani, washindani wao katika ligi hiyo Chelsea wakipepetana na mahasimu wao wa Ureno, Porto.
Hata hivyo, mechi nyingine kali itakuwa dhidi ya mabingwa mara saba Ulaya, AC Milan ambao kwa sasa kiungo wao Ronaldinho akiwa ameimarika itakaposaka nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano itakapoikaribisha Olympique Marseille.
Milan inayoshiriki Serie A inaongoza katika msimamo wa Kundi C, ikiwa pointi sawa na Real Madrid, lakini timu hiyo ya Ufaransa iko pointi moja nyuma ikiwa imebakiza michezo miwili kabla ya kufungwa kwa mechi hizo za makundi.
Mbali na mchezo huo, pia APOEL Nicosia leo ina kazi nyingine ya kupepetana na Atletico Madrid katika mechi ya kundi D.
VfL Wolfsburg inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi B ikiwa na pointi saba, itakuwa mgeni wa CSKA Moscow katika mchezo mwingine wa kundi hilo utakaozikutanisha timu mbili zenye uwezo wa kucheza hatua inayofuata.
Katika mechi za kundi A, Girondins Bordeaux itakuwa mwenyeji wa Juventus, Bayern Munich iliyokalia kuti kavu itaikaribisha Maccabi Haifa.

Ona sasa!

Javier Mascherano ya Liverpool, (chini) akidhibitiwa na mchezaji wa Debrecen, Gergely Rudolf (juu) wakati wa mechi ya ligi ya UEFA iliyochezwa kwenye uwanja wa Puskas mjini Budapest, jana. Picha: REUTERS

Hufungi hapa

KIPA wa Inter Milan, Julio Cesar (kushoto) akigombea mpira na mchezaji wa Barcelona, Thierry Henry wakati wa mechi ya ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa kwenye uwanja wa Nou Camp mjini Barcelona. Picha: Reuters

Liverpool 'out', Arsenal yapeta

LONDON, England
MABINGWA mara tano Liverpool jana walijikuta wakitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa kwenye hatua ya makundi pamoja na kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Debrecen huku Fiorentina na Arsenal wakifuzu kuingia kwenye 16 bora.
Mabingwa watetezi Barcelona walifufua kampeni yao kwa ushindi mzuri wa mabao 2-0 dhidi ya Inter Milan kwenye mechi iliyokuwa na mvuto zaidi usiku wa jana, wakijipatia mabao yao ndani ya dakika 26 za mwanzo kupitia kwa Gerard Pique na Pedro.
Arsenal wametinga hatua ya 16 bora kwa msimu wa 10 mfululizo kufuatia ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Standard Liege.
Fiorentina walifuzu baada ya kujipatia ushindi wa bao 1-0 kwa njia ya mchomo wa adhabu uliopigwa na Mperu Juan Vargas dhidi ya Olympique Lyon, ambao tayari wameshafuzu, na kujiunga na Girondins Bordeaux, Manchester United, Chelsea, Porto na Sevilla kwenye hatua inayofuata.
Ushindi wa Waitalia hao pia ulihitimisha ndoto za Liverpool za kufuzu kutoka kwenye Kundi E.
"Tumekuwa wazuri sana (kwenye miaka ya hivi karibuni) kwenye Ligi ya Mabingwa, sasa watu wanadhani itakuwa hivyo hivyo kila mwaka," meneja Rafa Benitez wa Liverpool aliwaeleza wanahabari.
Kikosi cha Benitez kiliwasili Hungary kikijua majaliwa yao kwa kiasi kikubwa hayakuwa mikononi mwao na goli la ushindi lililofungwa katika dakika ya nne na mshambuliaji Ngog, ambalo liliwafanya Debrecen wanaocheza michuano hiyo kwa mara ya kwanza kuchapwa mechi tano mfululizo, halikuweza kusaidia chochote.
Ushindi wa Fiorentina umewafanya waongoze kundi wakiwa na pointi 12, mbili juu ya Lyon huku Liverpool wakiwa nyuma zaidi kwa pointi tatu.
Hata kama mabingwa hao wa mara tano watalingana na Lyon, kikosi hicho cha Ufaransa kitafuzu kutokana na kuwa na rekodi nzuri walipokutana baina yao. Mshambuliaji wa zamani wa Barcelona Samuel Eto'o alipewa mapokezi mazuri aliporudi Nou Camp akiwa na klabu yake mpya ya Inter lakini mambo hayakuwa mazuri kwake.
Japokuwa Barcelona walikuwa wameshashinda mechi tatu tu kati ya saba zilizopita nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa, walikuwa hawajawahi kufungwa kwenye mechi sita dhidi ya timu za Italia.
Pamoja na kutokuwa na majeruhi Lionel Messi na Zlatan Ibrahimovic, Barcelona walikuwa wazuri sana kuwalinganisha na Inter.
Pique alifunga bao la kwanza kufuatia kona ya dakika ya 10 kabla ya Pedro kumaliza kazi kwa kupachika bao la pili dakika 16 baadaye.
Ushindi huo umewafanya Barcelona kuongoza Kundi F wakiwa na pointi nane, mbili mbele ya kikosi cha Jose Mourinho na walio nafasi ya tatu mabingwa wa Russia, Rubin Kazan, ambao walilazimishwa sare ya bila kufungana nyumbani na Dynamo Kiev.
Kiev wanashikilia mkia wakiwa na pointi tano lakini bado pia wanaweza kufuzu kwenye kundi hilo.
Barcelona watakuwa wageni wa mabingwa hao wa Ukraine kwenye mechi za mzunguko wa mwisho mwezi ujao huku Inter wakiwakaribisha Rubin.
"Tumeonyesha kwamba yeyote anayeingia kwenye kikosi hiki analeta kitu kipya," alisema Daniel Alves wa Barcelona akimaanisha watu waliochukuwa nafasi za Ibrahimovic na Messi.
Arsenal hawakuwa na kazi kubwa kuendeleza rekodi yao ya kutofungwa nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa dhidi ya timu za nje kufikia mechi 29.
Vijana hao wa London walijipatia mabao kupitia kwa Samir Nasri kwenye dakika ya 35 kabla ya Mbrazil Denilson kufunga kwa shuti la kutokea umbali wa mita 30 kwenye dakika za majeruhi za kipindi cha kwanza.
Ushindi huo umewahakikishia Arsenal nafasi ya kwanza kwenye Kundi H wakiongoza kwa tofauti ya pointi sita mbele ya Olympiakos waliotoka sare ya 0-0 dhidi ya AZ Alkmaar.
Unirea Urziceni walizidi kujipalilia nafasi zao kwenye Kundi G kwa kuwafunga Sevilla, ambao tayari wameshafuzu, kwa bao 1-0 baada ya Ivica Dragutinovic kujifunga mwenyewe kwa kichwa muda mfupi kabla ya mapumziko.
Mabingwa hao wa Romania wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi nane, mbili mbele ya VfB Stuttgart ambao waliwafunga Rangers mabao 2-0 kuwapa Wascotland hao kipigo chao cha tatu mfululizo kwenye kundi hilo.

Tuesday, November 24, 2009

Simba kwafukuta

Na Badru Kimwaga
WAKATI vuguvugu la uchaguzi mkuu Simba likizidi kushika kasi, limeibuka kundi la wanachama wa klabu hiyo na kutishia kuwafungia nje viongozi wao wa sasa ifikapo Desemba 4 mwaka huu.
Wanachama hao wakiongozwa na Issa Said Ruchaki 'Masharubu' mwenye kadi namba 2511, alisema wamedhamiria kufanya hivyo kutokana na ukweli mwisho wa uongozi huo unatakiwa kuhitimishwa Desemba 3.
Masharubu alisema watachukua hatua hiyo baada ya kuona viongozi hao wanataka kuwapiga 'changa la macho' juu ya uchaguzi mkuu, ambao unatarajiwa kutangazwa rasmi Jumamosi hii.
"Mkataba wetu na viongozi wa sasa wa Simba ni mwisho Desemba 3, baada ya hapo tutaifunga klabu na kuikabidhi timu kwa meneja Inoccent Njovu pamoja na manahodha Nico Nyagawa na Juma Kaseja chini ya Baraza la Udhamini la Wazee," alisema Masharubu.
Masharubu alisema anawakilisha kundi la wanachama zaidi ya 20, na kudai hawana tatizo na mtu yeyote bali wanataka klabu iwe chini ya watu hao hadi watakapopatikana viongozi wapya.
Aidha, alisema wanachama wa Simba wanawapa pongezi mwenyekiti Hassani Dalali na Mhazini Mkuu, Chano Almasi kwa kuendelea kugawa kadi za uanachama wa klabu hiyo bila ukomo kama walivyokuwa wamekubaliana.
"Hili la utoaji wa kadi hadi leo ni suala la kupongezwa kwani linafanya wawili hao wajiweke karibu na wanachama, ila msimamo wetu ni kwamba Desemba 3 ndio mwisho wa kukanyanga klabuni hadi viongozi wapya wapatikane."

FIFA kujadili bao la mkono la Henry

LONDON, England

SHIRIKISHO la Kimataifa la Soka Ulimwenguni-FIFA, linatarajia kufanya mkutano mwezi ujao, ambapo pamoja na mambo mengine litajadili tukio la kuucheza mpira kwa mkono lililofanywa na nahodha wa Ufaransa, Thierry Henry kwenye mechi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Lakini pia chombo hicho kikubwa chenye dhamana ya kusimamia mchezo wa soka, kitajadili vurugu zilizotokea kwenye mechi kati ya majirani wawili, Misri na Algeria wiki iliyopita.
FIFA mpaka sasa imekataa kuchukua hatua zozote dhidi ya Henry anayetuhumiwa kuucheza mpira kwa mkono na kupelekea bao la kusawazisha kwa Ufaransa wakati ikicheza na Ireland.
Chama cha soka cha Ireland kiliomba mechi hiyo kurudiwa, hata hivyo ombi lao halikukubaliwa.

Vigogo vya Soka Ulaya dimbani leo

Ni Liverpool, Barca, Bayern
LONDON, England

Vigogo Barcelona, Liverpool na Bayern Munich leo zenye rekodi ya kutwaa ubingwa wa vilabu barani Ulaya, ziko katika hatari ya kutolewa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya leo na kesho.
Mabingwa watetezi Barcelona watakabiliana na mshambuliaji wao wa zamani Samuel Eto'o katika pambano lao dhidi ya Inter Milan na endapo itafungwa, huku timu ya Russia ya Rubin Kazan itaibuka na ushindi dhidi ya Dynamo Kiev, itakuwa imefungasha virago katika mashindano hayo.
Liverpool nayo leo iko katika hatari ya kutupwa nje kwa vile hata kama itashinda, bado kuendelea kwake mbele kwenye michuano hiyo kutategemeana matokeo ya timu zingine, endapo Fiorentina itaifunga Olympique Lyon ambayo tayari imeshafuzu, basi safari ya Liverpool itakuwa imeiva.
Miamba mingine ya Ujerumani, Bayern Munich ambayo itakuwa nyumbani ikicheza dhidi ya Maccabi Haifa ikijua kuwa, hata wakishinda kama wanavyotarajiwa watatupwa nje endapo Juventus itaifunga Girondins Bordeaux ambayo tayari imeshafuzu katika hatua ya timu 16 bora.
Katika mechi zingine, Arsenal itaungana na Lyon, Bordeaux, Chelsea, Porto, Manchester United na Sevilla katika hatua hiyo ya mtoano inayoshirikisha jumla ya timu 16 wakati AC Milan na Real Madrid pia zina nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mashindano hayo.
Inter itakuwa mgeni wa Barcelona katika mchezo wa Kundi F utakaofanyika leo, ambao unakodolewa macho na wengi.
Waitalia wanaoongoza kundi hilo baada ya kuifunga Dynamo Kiev katika mchezo wa mwisho wiki mbili zilizopita, ikiwa na pointi moja zaidi ya Rubin Kazan na Barcelona huko Waukraine wakiwa nyuma zaidi.
Kiosi cha kocha Pep Guardiola kilikimbilia kumpata Zlatan Ibrahimovic na Lionel Messi amerejea katika ubora wake kwa ajili ya mchezo huo muhimu sana.
Mshambuliaji wa Argentina Messi alipata maumivu ya misuli Jumamosi wakati wakati timu yake ikitoka sare ya 1-1 na 1-1 katika mchezo wa La Liga huko Athletic Bilbao na Ibrahimovic aliukosa mchezo huo, kutokana na maumivu kama hayo.
Beki Eric Abidal na kiungo Yaya Toure wameambukizwa virusi vya homa ya mafua ya nguruwe lakioni Guardiola alikataa kupiga mayowe kuhusu matatizo yaliyomo katika kikosi chake.
"Endapo wachezaji hao hawatakuwepo...tutawatumia wachezaji wengine. Kamwe huwezi kutwaa taji ukiwa na wachezaji wawili au watatu tu, "alisema baada ya mchezo dhidi ya Bilbao.
Bayern Munich bado haijawahi kushinda mchezo wowote nyumbani katika Kundi A na , licha ya kesho Jumatano kuwa na kibarua chepesi kufuatia kupangwa kucheza na timu isiyo na uwezo sana ya Maccabi kesho, lakini imechelewa kuibuka.
Liverpool, ambayo inaweza kuzikosa fainaloi za msimu huu, tayari wamemkosa mshambuliaji wake muhimu Fernando Torres kwa ajili yamchezo wa leo Jumanne utakaopigwa Hungary katika Kundi E.
Timu ya kocha Rafael Benitez iko katika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi lake ikiwa na pointi nne, tano nyuma ya Fiorentina.
Kushindwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo kutaifanya Liverpool kuondolewa mapema endapo Fiorentina itaibuka na ushindi dhidi ya Lyon.
Vinara wa Kundi C Milan itafuzu hatua hiyo ya mtoano endapo itaifunga Olympique Marseille nyumbani kesho Jumatano.
Ushindi wa Milan pia utaiwezesha Real Madrid kufuzu mradi tu iwafunge mabingwa wa Uswisi FC Zurich, ambayo tayari iliteleza kwa kufungwa bao 12 baada ya kucheza mechi 12 na kufungwa 5-2 nyumbani dhidi ya klabu ya Hispania katika mechi za mapema.
Milan na Real - ambazo uwanja wao wa Bernabeu utaandaa fainali za Ligi ya Mabigwa wa Ulaya msimu huu, kila moja ina pointi saba, moja juu ya Marseille.

Monday, November 23, 2009

Yanga yamchanganya Micho

Na Jacqueline Massano

BAADA ya uongozi wa klabu ya Yanga ya Jijini kutangaza kuwaacha wachezaji watano akiwemo mshambuliaji mkenya Boniface Ambani, aliyewahi kocha mkuu wa timu hiyo, Milutin Sredejovic 'Micho' amesikitishwa na hatua hiyo.
Akizungumza na Alasiri kwa njia ya simu jana, Micho huyo ambaye kwa sasa anaifundisha timu ya St. George ya Ethiopia amesema Yanga kwa kuwatema wachezaji hao imepotea njia.
Wiki iliyopita, klabu hiyo bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara imetangaza kuwatema wachezaji watano akiwemo Ambani, Joseph Shikokoti, George Owino, Yusuf Hamis na Vincent Barnabas ambaye amewekwa 'bondi' African Lyon.
"Hawa Yanga, naona wameanza kuishiwa kwa nini wameawaacha wachezaji hao wakati ni wazuri... ni nini kimewasibu," alihoji kocha huyo wakati akizungumza na Alasiri.
Kocha huyo alisema kama Yanga imeamua kuwaacha wachezaji kwa sababu ya kushuka kiwango chao."Hivi ni kweli wachezaji hawa kiwango chao kimeshuka, au hawana nidhamu, nataka nijue kwa undani zaidi. Kwanini wameachwa, mimi sijui ila kwa sababu ya kiwango, sina hakika.
"Na kama inawezekana naomba nipe namba ya Ambani ili nizungumze naye nipate jinsi ya kumsaidia, tafadhali fanya hivyo," aliongeza kocha huyo.
Hata hivyo, Alasiri ilipozungumza na Ambani kutaka kufahamu kama amewasiliana na kocha huyo alisema: "Bado hatujawasiliana."
Ambani alisema kwa sasa ameanza taratibu za kutafuta timu nje ya nchi na muonekano unaonyesha mafanikio katika zoezi hilo.
"Kama Yanga wameniacha sijali, kwa sababu nimeanza taratibu za kutafuta timu nje yaBongo," alisema Ambani.

Laazizi wa Britney jela siku 45

LOS ANGELES, Marekani
MPIGA picha aliyewahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa muda mfupi na msanii Britney Spears, amehukumiwa kwenda jela siku 45 baada ya kupatikana na hatia ya kukwaruzana na afisa mmoja wa polisi.
Adnan Ghalib, 37, aliyekuwa karibu na mrembo huyo msanii wa muziki mwaka 2007, mbali na kifungo hicho pia ametakiwa kushiriki katika mafunzo ya kuzuia na kudhibiti hasira.
Mwendesha mashitaka wa Los Angeles, alisema Februari mwaka huu, Ghalib alikiuka agizo la mahakama lililomtaka kuwa mbali na Spear na familia yake, na aliposimamishwa na afisa huyo alianza kukwaruzana naye.
Mwenyewe Ghalib alikiri shitaka hilo, lakini kosa lingine alilofunguliwa kutokana na tukio hilo lilifutwa.
Spears, 27, alianza mahusiano ya kimapenzi na Ghalib Desemba 2007 wakati huo msanii huyo akiwa kwenye wakati mgumu kufuatia mtafaruku uliopelekea kupewa talaka na aliyekuwa mme wake.

Beckham anogewa na soka

LONDON, England
David Beckham amesema ataendelea kucheza soka England hata baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Afrika Kusini.
"Kama tutashinda Kombe la Dunia na kufikia rekodi, litakuwa jambo zuri kumaliza, lakini bado naona ni ngumu kuacha kucheza," alisema kiungo huyo wa L.A. Galaxy ya Marekani.
"Hata kama ndoto yangu itakuwa ya kweli, bado nitaendelea kucheza kwenye nchi yangu. Ningependa niendelea kushiriki kwa njia moja ama nyingine."
Hamu yangu kwa timu na nchi ni kubwa, na hii haitabadilika," aliongeza Beckham ambaye atafikia rekodi sawa na kipa wa Englansd Peter Shilton ya mechi 125 kama atacheza mara kwa mara kwenye fainali za mwakani.

Friday, November 20, 2009

Utamu wa Kombe la Dunia

Rais, Jakaya Kikwete akihutubia mara baada ya kuwasili kwa kombe la Dunia jana.
Haya na huyu kaka wa Alasiri, Daniel Mkate alikuwepo kwenye hafla hiyo iliyofanyika kwenye uwanja huo. Kasoro mimi tu sikuhudhuria.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) akitaka kumpa Kombe la Dunia mke wake, Salma Kikwete wakati wa hafla hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa. Hata imefahamika kuwa kombe hilo halilihusiwi kushikwa na mtu mwingine zaidi ya Rais wa nchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) akiwa na Kombe la Dunia, wakati wa shamrashamra zilizofanyika jana kwenye uwanja wa Taifa, Dar.

JK 'amuua' Tenga

Na Daniel Mkate, U/Taifa
BAADA ya kuteta kirafiki na Rais wa Shirikisho la Soka nchini, TFF, Leodger Tenga, kabla hajapanda jukwaani kulipokea Kombe la Dunia, Rais Jakaya Kikwete, 'alimuua' bila aibu kiongozi huyo wa soka kuhususiana na mwenendo wa shirikisho lake.
Akizungumza baada ya kupewa nafasi kuhutubia shamrashamra za kulikaribisha kombe hilo, JK alisema TFF limeonekana kuwa shirikisho la ushabiki na mapato pekee yake badala ya kuendeleza soka.
"Ulegevu wa TFF ni ushabiki na mapato pekee, sijui inakuwaje katika kuendeleza soka nchini...mwenendo huu ukiendelea hivi lazima tutadumaa na tutaendelea kusimamia ligi kuu pekee," alisema JK na kumuacha Tenga akifurahi shingo upande.
JK alisema pamoja na shirikisho hilo kuonekana kuendeshwa kwa misingi hiyo, lakini bado limeonekana la kipekee ulimwenguni kwa kutoa adhabu za kukomoa wachezaji.
"Naona ajabu sana, mchezaji akifanya kosa anafungiwa miezi sita, jamani hizo adhabu mmezitoa wapi...kwanini asifungiwe mechi tatu na fani juu yake, tunahitajai vijana wetu wacheze soka na si kukomoana," alishangaa JK.
Pamoja na kulishukia shirikisho hilo, pia JK alizipiga dongo klabu kubwa nchi za Simba na Yanga kuhusiana na kutojenga misingi ya soka la vijana na kukimbilia kushindana kununua wachezaji kwa bei mbaya.
Alisema soka la vijana ndio msingi mkubwa, lakini klabu zetu hizi kubwa (bila kuzitaja) zisiogopwe pale TFF inapojenga misingi yake.
"Klabu jengeni vipaji , tuwekeze katika soka la umri mdogo...tafuteni walimu wazuri na wala si wachambuzi wa soka ili kuendeleza soka," alisema.
Kombe la Dunia lipo nchini kwa ziara ya siku tatu ambayo inamalizika rasmi kesho huku pia wakazi wa visiwa vya Unguja wakipata nafasi ya kuliona.

Shamrashamra za Kombe la Dunia uwanja wa Taifa

Anko Faustine naye alikuwepo kwa ajili ya kuripoti kwenye gazeti la Nipashe
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera (katikati) akiteta jambo na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete (kulia). Kushoto, ni Rais wa Shirikisho la Soka nchini, TFF, Leodgar Tenga.

Msafara wa pikipiki ukiingia kwenye uwanja wa Taifa.


Helikopta iliyokuwa inalinda usalama wa Kombe la Dunia, ikirandaranda maeneo ya uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.



Screen ya uwanja mpya wa Taifa ikionyesha jinsi ndege iliyobeba kombe la Dunia inavyotua.

Wachezaji wadundana uwanjani

RIO DE JANEIRO, Brazil

WACHEZAJI wawili wa timu ya Palmeiras Obina na Mauricio wametimuliwa na uongozi wa timu hiyo baada ya kupigana uwanjani, na kisha refa kuwalima kadi nyekundu kwa utovu huo wa nidhamu.
Wawili hao walichapana makonde wakati wakitoka uwanjani kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mapumziko katika mechi waliyofungwa mabao 2-0 na Gremio.
Kwa kosa hilo, Palmeira walilazimika kucheza wakiwa tisa uwanjani kwa kipindi chote cha pili.
"Wachezaji hawa hawatacheza tena soka na Palmeiras," alisema makamu wa rais Gilberto Cipullo wakati akiongea na waandishi wa habari.
Mshambuliaji Obina na mlinzi Mauricio walikuwa wakibishana kufuatia bao la kuongoza la Gremio lililofungwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza na Rafael Marques.
Wakati wanatoka kwa ajili ya kwenda kupumzika kwenye uwanja wa Olimpiki mjini Porto Alegre, ghafla walianza kupigana ngumu kabla ya kutenganishwa na wachezaji wenzao. Lopez alifunga bao la pili kwa Gremio katika dakika ya 70.

Wednesday, November 18, 2009

Yanga yadaiwa mil. 21

Na Jacqueline Massano

KOCHA msaidizi wa klabu ya mabingwa wa soka nchini-Yanga, Spaso Sokolovisk, ambaye mkataba wake umefikia ukomo katikati ya mwezi huu, anaidai klabu hiyo ya Jangwani shilingi milioni 21.
Kiasi hicho ni malimbikizo ya mishahara ya miezi minne, kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo Alasiri imezipata mapema leo.
"Kwanza ni kweli, Spaso anaidai klabu yetu shilingi milioni 21,440,000 ambazo ni malimbikizo ya mishahara ya miezi minne," alisema mtoa habari ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.
"Hivi sasa viongozi wanaangalia namna ya kupata fedha hizo na kumkabidhi. Tunafahamu mkataba wake umeshakwisha," alisema zaidi.
Akifafanua zaidi, alisema: "Kwa mwezi tulikuwa tunapaswa kumlipa kiasi cha shilingi milioni 5,360,000. Haya ni makubaliano yaliyoko kwenye mkataba."
Bosi wa kitengo cha habari cha klabu hiyo, Louis Sendeu, alikiri kocha huyo kuidai klabu yake, lakini hakuwa tayari kukiri kiasi cha shilingi milioni 21 wanazodaiwa.
"Kweli anatudai, hakuna kificho kwenye hili, tunafanya utaratibu wa kumlipa mapema kama alivyodai," alisema na kuongeza: "Siwezi kusema tunadaiwa kiasi gani, ila kama yeye mwenyewe (Spaso) yuko tayari kusema ni kiasi gani, afanye hivyo."
Bosi Sendeu alimtaka kocha huyo kutulia wakati taratibu za malipo yake zikiandaliwa. "Ninamshauri kuwa mvumilivu, suala lake linajulikana tangu mkataba wake ulipomalizika Nov. 15," aliongeza.
Kutokana na kuchelewa kulipa kwa wakati ,Yanga imejikuta ikiandamwa na madeni mengi, ambapo baada ya mkataba wa kocha wa kwanza, Dusan Kondic kumalizika, klabu hiyo ilijikuta ikidaiwa zaidi ya shilingi milioni 30.

Mabao 177 yazamishwa ligi kuu Bara

Na Adam Fungamwango

MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara umemalizika kwa timu zote 12 kucheza mechi 11, huku magoli 177 yakiwa yamepachikwa nyavuni.
Magoli hayo yamefungwa na wachezaji 84 kati ya 323 wanaoshiriki Ligi hiyo kwa michezo 66 ambayo imechezwa, huku magoli 11 yakifungwa kwa mikwaju ya penati.
Pia, takwimu zinaonyesha kuwa raundi ya 11 ambayo ni ya mwisho kwa mzunguko wa kwanza, imevunja rekodi kwa kuwa na magoli mengi kuliko raundi zote za nyuma.
Kabla ya raundi ya 11, raundi ya kwanza ndiyo iliyokuwa na idadi kubwa ya magoli.
Takwimu zinaonyesha kuwa mechi za raundi ya kwanza ambazo zilikuwa za ufunguzi wa Ligi Kuu yalipatikana magoli 19 na idadi hiyo haikuvukwa na raundi zote zilizofuata hadi raundi ya 11 ya kufunga mzunguko wa kwanza ambapo magoli 27 yamepatikana.
Ushindi wa JKT Ruvu wa mabao 4-2 dhidi ya African, Majimaji kuitungua Moro United mabao 3-2, Toto kuitundika Kagera Sugar 2-0, Azam kuisulubu Manyema mabao 4-0, Simba kuitandika Mtibwa Sugar 3-1 na Yanga kuisasambua Prisons mabao 4-2, kumefanya idadi ya magoli kuwa 27 na kuvunja rekodi ya raundi zote.
Kwa upande wa wafungaji, John Bocco wa Azam FC anaendelea kuchanja mbuga ambapo kwa sasa amefikisha magoli tisa na kuzidi kujiwekea mazingira mazuri ya kuwa mfungaji bora mwaka huu.
Hata hivyo anafukuzwa kwa washambuliaji wawili, Hussein Bunu wa JKT Ruvu na Mussa Hassan 'Mgosi' wa Simba ambao wana magoli sita kila mmoja, huku Mrisho Ngassa wa Yanga na Yusuph Soka wa African Lyon wao wakiwa na magoli matano.
Wachezaji Yahaya Tumbo wa Azam, Jerryson Tegete wa Yanga na Yona Ndabila wa Moro United wao wana magoli manne, huku Mbwana Samata wa African Lyon, Danny Mrwanda wa Simba, Michel Katende wa Kagera Sugar, Benedict Ngassa wa Manyema, Maulidi Haniu wa Toto African na Kigi Makasi wa Yanga wakiwa na magoli matatu kila mmoja.

Algeria, Misri uso kwa uso leo

KHARTOUM, Sudan
Wachezaji wa Algeria, wamesema wako fiti kwa asimilia 100 kukabilina na Misri mjini Khartoum, Sudan katika mechi muhimu ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia, 2010-Afrika Kusini.
Baada ya mechi ya Jumamosi kujawa na vurugu, maelfu ya mashabiki kutoka Algeria na Misri wamewasili mjini Khartoum kushuhudia mechi hiyo, ambapo katika hali ya kuimarisha ulinzi, askari 15,000 watakafanya kazi hiyo.
"Timu yote iko kamili kwa ajili ya vita hii," alisema mlinzi wa Algeria, Madjid Bougherra anayecheza soka ya kulipwa na klabu ya Rangers.
"Kila mchezaji yuko fiti." Alisema, mlinzi anayecheza timu ya VfL Bochum, Antar Yahia, atacheza mechi ya leo baada ya kupata nafuu.
Kocha wa Misri Hassan Shehata, ambaye bado ana imani na kikosi chake kufuzu kufuatia kuibuka na ushindi kwenye mechi ya kwanza, huku bao la ushindi likifungwa kwa kichwa na Emad Moteab dakika tano kabla ya kumalizika mchezo, amesema atatumia mbinu nyingine ili kupata ushindi

Tuesday, November 17, 2009

Namba ya Papic ya uanachama ni 7696

KOCHA mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amechukua kadi ya uanachama wa klabu hiyo, ambapo anatarajiwa kukabidhiwa kadi yake mara atakaporejea kutoka Serbia alipokwenda kwa ajili ya mapumziko mafupi.

Cheka na Msamba


Yanga yaichakaza Prisons 4-2


Monday, November 16, 2009

Yanga uso kwa uso na Maafande wa Prison


MABINGWA wa soka wa Ligi ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga, leo wanatarajia kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kwa kumenyana na Prisons ya Mbeya kwenye mechi itakayochezwa uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo ambayo itakuwa ni ya vuta ni kuvute, Yanga inaingia uwanjani ikiwa katika nafasi ya nne na pointi 18 huku Prisons ikiwa pointi nane ikiwa nafasi ya 10.
Ili ziweze kufanikiwa kupanda katika msimamo wa ligi, timu hizo mbili zote kwa pamoja zitaingia uwanjani huku zikiwa na hamu ya kufanikiwa kuibuka na pointi tatu ili ziweze kupiga hatua mbele.
Ikiwa Yanga itafanikiwa kushinda katika mchezo huo, moja kwa moja itapanda hadi nafasi ya tatu huku ikiiacha Mtibwa Sugar katika nafasi ya nne.

Yanga: Nurdin aendi popote

UONGOZI wa klabu ya soka ya Yanga, umedai mchezaji wao kiungo Nurdin Bakari, hawana mpango wa kumtoa kwa timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu Bara kutokana na mkataba wake wa miaka miwili kutomalizika.
Afisa Habari wa timu hiyo, Louis Sendeu, amesema licha ya habari zilizoenea Jijini kuwa mchezaji huyo anafukuziwa na Simba, lakini uongozi wa wana Jangwani hauna mpango wa kumtoa.
"Iwapo Simba wanamuhitaji mchezaji huyo wasifanye papara za kuzungumza naye, kwani bado ana mkataba nasi kwa kipindi cha miaka miwili ijayo, hivyo wasikurupuke kama wamempata Mike Barasa ni huyo huyo wala si Nurdin," alisema Sendeu.
Sendeu alisema mchezaji huyo kwa hivi sasa hana mpango na Simba kutokana na kumuacha katika usajili miaka miwili iliyopita kwa kile kilichoelezwa matatizo ya moyo.
"Kwa sasa Simba wamesahau kama walimuacha mchezaji huyo kwa sababu ya matatizo ya moyo, sasa iweje waanze kumnyatia tena," alihoji msemaji huyo.
Habari zinasema baada ya Simba kufanikiwa kumnasa mchezaji Mkenya, Mike Barasa, kwa sasa wamemgeukia kiungo huyo ili kuimarisha kikosi chao katika dirisha dogo la usajili baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kumalizika leo wakati Yanga itakapocheza na Prisons ya Mbeya.
Hata hivyo, Sendeu alisema iwapo Simba wanamtamani mchezaji huyo, wanatakiwa kuwasiliana na uongozi wa klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani ili kufanya mazungumzo ya 'kujenga'.
Mchezaji huyo alivutiwa na aliyekuwa kocha mserbia wa Yanga, Dusan Kondic, licha ya matatizo yake ya moyo yaliyodaiwa na Simba, hata kumshawishi kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo kumuita katika kikosi chake.

Diego 'jela' miezi 2

ZURICH, Uswisi
KOCHA wa timu ya taifa ya Argentina, Diego Maradona amefungiwa kutojishughulisha na soka kwa muda wa miezi miwili na kutozwa faini zaidi ya shilingi milioni 24 kufuatia kauli alizotoa wakati wa mechi ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Afrika Kusini.
Maradona, 49, aliomba radhi kwa kauli alizotoa, kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, FIFA.
Maradona anatuhumiwa kutoa maneno machafu wakati akihojiwa 'live' na kituo cha televisheni wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Kocha huyo aliyechaguliwa kufundisha timu ya taifa ya Argentina miezi 13 iliyopita baada ya muda mrefu wa ushauri na matibabu ya kuacha kutumia dawa za kulevya na ulezi wa pombe, aliitwa na kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu ya FIFA.
"Kamati ya nidhamu ya FIFA leo hii imeamua kumpa adhabu ya miezi miwili kutojihusisha na soka na faini ya shilingi milioni 24 kocha wa timu ya taifa ya Argentina Diego Maradona," ilisema taarifa ya FIFA.
"Kamati imetupilia mbali ombi la msamaha la Maradona.
"Kamati imeonya, endapo Maradona atarudia tena utovu wa nidhamu kama huo, ina maana kwamba atakabiliwa na adhabu zaidi."FIFA imesema adhabu hiyo inaanza mara moja na kwamba itamalizika Januari 15.
Hii ina maana kwamba, Maradona hatakosa mechi za mashindano, bali atakuwa ndani ya adhabu wakati kikosi chake kikicheza na timu ya taifa ya Czech katika mechi ya kirafiki mwezi ujao.

Friday, November 13, 2009

Barasa aikimbia Simba, Yanga

Jacqueline Massano

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Yanga, amendoka leo kurejea kwako, Nairobi nchini Kenya na kuziacha kwenye mataa klabu za Simba na Yanga.
"Nimeamua kuondoka kurudi nyumbani (Kenya) baada ya kuona hakuna la maana walilosema viongozi wa Yanga," alisema mchezaji huyo wakati akiongea na Alasiri mapema leo.
"Naona haipo sababu ya kuendelea kukaa hapa (Tanzania) bila kuwa na kazi ya kufanya, nimeamua kurudi nyumbani. Mwenye shida na mimi, nadhani atalazimika kwanza kunitafuta toka Kenya," aliongeza zaidi.
"Navyozungumza na wewe napanga mizigo yangu ili niondoke, mambo yakienda vizuri usiku nitakuwa Nairobi," alisema zaidi mshambuliaji huyo ambaye kwa wiki nzima amekuwa gumzo kwenye vyombo mbalimbali vya habari.
Kulikuwa na taarifa kwamba, nyota huyo wa Kenya amekuwa akiwakwepa viongozi wa Yanga, lakini mwenyewe alipoulizwa hilo alisema: "Kuna maneno ya mitaani, ndio kama hayo unayoniuliza. Kwanini niwakwepe?. Eti nataka kukimbia, kwenda wapi, na ili iweje?"
"Niko tayari kurejea tena, kama kuna timu inanihitaji---Simba au Yanga, zinanihitaji ni suala la makubaliano tu," alisema zaidi.
Aidha, Barasa amesema amefanya mazungumzo na viongizi wa Simba lakini hawajafikia makubaliano na taarifa kwamba amesaini mkataba hazina ukweli.

kauli zamponza Fergie, atupwa selo

LONDON, England
KOCHA wa Manchester United, Alex Ferguson amelimwa adhabu 'nene' ya kutokaa kwenye benchi kwa mechi nne pamoja na faini ya zaidi ya shilingi milioni 30, taarifa ya Chama cha Soka England, (FA) ilisema jana.
Kwa adhabu hiyo, kocha huyo mkali wa kutoa maoni Ligi Kuu England, atatumikia mechi mbili, na kisha mechi zingine mbili anaweza kuongezewa iwapo katika kipindi cha kutumikia adhabu ya mechi mbili za kwanza atafanya kosa lingine.
Lakini kama hatopatikana na kosa lingine, ina maana adhabu yake itakuwa kutumia mechi mbili tu.
Adhabu ya Ferguson imetokana na kauli aliyotoa dhidi ya refa Alan Wiley, aliyemtuhumu kutokuwa na uwezo wa kuchezesha soka wakati alipochezesha mechi kati ya timu yake na Sunderland mwezi uliopita.
Wakati wa kusikiliza shauri lake mjini London, Ferguson, 67, alikiri kutoa kauli hiyo katika mechi iliyomalizika kwa sare ya 2-2 kwenye uwanja wa Old Trafford.
Ferguson alisema Wiley hakuwa na uwezo wa kuchezesha mechi hiyo. Bosi wa tume ya usimamizi, Peter Griffiths, alisema hakuna mashaka kwamba Alex Ferguson alitoa kauli hiyo, ambayo kimsingi hakupaswa kama mwanamichezo.
Alan Leighton, mkuu wa umoja wa marefa, alimtuhumu Ferguson kwa utovu huo wa nidhamu. Ferguson alimponda Wiley wakati wa mahojiano na kituo cha televishen akisema: "Hakuwa kwenye kiwango cha kumchezesha soka."
Ferguson pia aliwahi kutoa maneno yasiyofaa kwa refa Martin Atkinson wakati Manchester United wakifungwa bao 1-0 na Chelsea katika mechi ya Ligi Kuu Jumapili. "Wakati mwingine unakosa imani na refa, ndivyo wanavyosema wachezaji," alisema mara baada ya mechi kumalizika.
Hata hivyo FA, imesema Ferguson hatakumbwa na adhabu kutoka Shirikisho la Soka la Ulimwenguni-FAFA kwa matamshi yake.

Mrembo adakwa na 'unga'

LONDON,England
Mwanamitindo Kelly Askew, amakamatwa akiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani ya paundi 627,000.
Dawa hizo zilikamatwa kwenye gari lake, polisi walisema. Wakati anakamatwa alikuwa kwenye gari lake aina ya Mercedes Benz lenye thamani ya paundi 12,000, sambamba na mpenzi wake John Clayton.
Walikamatwa karibu na barabara inayounganisha Bradford na West Yorks, mapema jana. Kabla ya kukamatwa walionekana wakikutana na mtu mmoja, taarifa zaidi zilidai.
Kisha polisi waliweka kizuizi na kuwakamata karibu na Bolton na kuwakuta wakiwa na kilo mbili za Cocaine ya kiwango cha juu. Askew, anayeishi Liverpool, alisema hajui lolote kuhusu mzigo huo, na kwamba mara nyingi amekuwa akimuendesha mpenzi wake kwa vile ana adhabu ya kutoendesha gari. Lakini polisi walisema simu ya kwenye gari ilionyesha kuwepo kwa mawasiliano kati ya Askew na Clayton, ambaye alikiri kumiliki mzigo huo.

Wachezaji Algeria washushiwa mvua za mawe

ALGIERS, Algeria
WACHEZAJI watatu wa timu ya taifa ya Nigeria, wamepata majeraha madogo baada ya basi walilopanda wakati wakiwasili mjini Cairo kushambuliwa kwa mawe na vijana, radio ya taifa ya Algeria ilitangaza jana.
Waziri wa mambo ya nje ya Algeria, amelaani tukio hilo ambalo limefanyika siku tatu kabla ya mechi muhimu itakayoamua ni timu gani kati ya Misri na Algeria itakayokwenda kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Afrika Kusini.
Taarifa zinasema kuwa, karibu vijana 200 walikuwa sehemu karibu na hotel ambayo timu hiyo ilipanga kufikia na kisha kurusha mawe kuelekea kwenye basi na kuvunja vioo kadhaa.
"Ni tukio baya la kujutia," alisema waziri wa Vijana na Michezo wa Algeria, Hachemi Djiar.
"Lakini pia basi lilipotoka uwanja wa ndege, vijana wengine pia walifanya shambulizi la mawe," aliongeza.
Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa na viongozi wa Misri kuhusu tukio hilo.
Waziri anayehusika na dhamana ya michezo wa Algeria, alisema FIFA wana taarifa za tukio na walikuwa wakikutana kuamua nini cha kufanya.
Mechi ya Misri na Algeria inatarajia kuwa na upinzani mkali, kwani kama Algeria watashinda basi watakwenda kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu waliposhiriki mara ya mwisho mwaka 1986.
Kushindwa kufuzu kwa Misri kwenye fainali za mwakani kutakuwa pigo kubwa kwao hasa ukizingatia kuwa wao ndio mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika.

Thursday, November 12, 2009

Simba: Yanga karibuni mnuso

Na Adam Fungamwango
WANACHAMA wa Simba tawi la Mburahati kwa Jongo, mwishoni mwa wiki iliyopita walitimiza ahadi yao ya kupika pilau na kula pamoja na wenzao wa Yanga kama sehemu ya furaha ya ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya watani wao wa jadi Oktoba 31 kwenye uwanja wa Taifa.
Mwenyekiti wa Simba tawi la Lion SC la Mburahati kwa Jongo, Abdallah Kipaga, amesema kuwa wameamua kuangusha pilau na kuwakaribisha watani wao baada ya kuwachapa, kutokana na utamaduni waliojiwekea tangu mwaka 2003.
"Sisi Simba tawi la huku na Yanga, tulikaa na kuwekeana utaratibu kuwa timu moja ikishinda, basi wanachama wake watalazimika kuwapikia wenzao pilau ikiwa ni kama njia ya kuwakoga na kuwafariji, hii ilikuwa mwaka 2003 na ndivyo tunavyofanya huku," alisema Mwenyekiti huyo.
Amesema kuwa moja kati ya masharti ambayo wamepeana ni waliofungwa ndiyo wanaokwenda kuchagua mbuzi ambaye atatumika kwenye shughuli hiyo, lakini nao sharti lao ni mwamba wachague mbuzi jike kwa sababu wamefungwa.
"Kwa kweli wikiendi iliyopita tumewalisha Yanga wote wa tawi la Mburahati wa Jongo pilau na utaratibu wetu ni kwamba wao wanakaa tu, sisi kwa sababu tumeshinda ndiyo tunapika, tunawaandalia na tunafanya utani," alisema Kipaga.
Hata hivyo amesema kuwa mwaka jana wenzao hawakuwafanyia hivyo baada ya kuwafunga bao 1-0 na walipowauliza walisema kuwa hali yao ya kiuchumi haikuwa nzuri.
Kipaga amesema kuwa wametumia kiasi cha sh 230,000 kufanikisha hafla hiyo, lakini amesema katika masharti yao timu zikitoka sare hakuna mtu wa kumlisha mwenzake pilau.

Dunga aimalisha kikosi cha 'kuiua' England

SAO PAULO, Brazil
KOCHA Dunga amemuita kwenye kikosi cha Brazil mlinzi wa AC Milan, Thiago Silva kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya England wiki ijayo.
Silva anajiunga na kikosi hicho kuchukua nafasi ya mlinzi wa Benfica, Luisao kufanyiwa upasuaji mdogo wa kidole cha tumbo.
Milan imekubali ombi la kufuatia muda wa kuruhusu wachezaji kufika, lakini ikifanya hivyo pia kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na Shirikisho la Soka Brazil, kwa mujibu wa taarifa zilizotumwa kwenye tovuti ya klabu hiyo jana.
Luisao alifanyiwa upasuaji jana, na kuamua kujiondoa kwenye kikosi cha Brazil kwa ajili ya mechi dhidi ya England itakayochezwa mjini Doha.

Wachezaji wamchanganya Papic

Na Jacqueline Massano
UONGOZI na kocha mkuu wa klabu ya Yanga, hadi sasa hawajui nani watamuongeza katika usajili wa dirisha dogo la Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia wachezaji wote walioanza majaribio na klabu hiyo kufanya vizuri.
Isitoshe, bado haijafahamika mchezaji gani atakayepunguzwa kwenye kikosi hicho kutokana na wachezaji wote kuwa na mkataba na klabu hiyo isipokuwa Mike Barasa ambaye mkataba wake umemalizika.
Yanga ina nafasi moja tu ya kuongeza mchezaji iwapo itashindwa kukubaliana na mshambuliaji wa kimataifa, Barasa ili aweze kuongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo.
Habari zilizopatikana mapema leo ni kwamba, hadi sasa kocha wa timu hiyo, Kostadin Papic hajajua ni mchezaji gani amsajili kwenye timu yake kwa sababu bado anamuhitaji Barasa na pia amevutiwa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Salvatory Edward
.Habari zinadai kuwa baadhi ya viongozi wameonyesha nia ya kutaka kumsajili tena aliyekuwa kipa namba moja wa klabu hiyo, Ivo Mapunda ambaye alikuwa anaichezea St. George ya Ethiopia.
"Haya ni maajabu, maana hadi sasa haijajulikana nani anapunguzwa na nani anaongezwa, kwani kocha naye anamtaka Barasa aendelee kuitumikia klabu hiyo. Uongozi pia unamtaka Ivo," alisema mtoa habari ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.
Yanga iko kwenye mchakato wa usajili mdogo ingawa hadi sasa haina nafasi ya kuongeza mchezaji, vinginevyo kama watapunguza wachezaji kwenye kikosi chao.

Wednesday, November 11, 2009

Kipa Ujerumani agongwa na treni

BERLIN, Ujerumani
KIPA wa timu ya taifa ya Ujerumani na Hanover 96, Robert Enke, amefariki papo hapo baada ya kugongwa na treni iendayo kwa kasi, tukio linaloonekana kama la kupanga kujiua mwenyewe, taarifa ya polisi ilisema jana usiku.
"Ushahidi wa awali unaonyesha alipanga kujiua, "afisa habari mdogo wa polisi, Lower Saxony alisema wakati akiongea na Reuters, kabla ya kuongeza kwa kusema mwili wa kipa huyo ulikutwa karibu na makutano ya reli katika mji wa Neustadt, Hanover.
"Majira ya jioni, aligongwa na treni ya kasi inayosafiri kati ya mji wa Hamburg na Bremen," msemaji mwingine wa polisi, Stefan Wittke alisema.
"Treni ilikuwa kwenye kasi ya kilomita 160-kwa saa." Wachezaji na marafiki zake, na mshauri Joerg Neblung waliwaambia waandishi wa habari "Nawedha kuthibitisha tukio hili ni la kujiua mwenyewe.
Aliamua kujiua mwenyewe kwa kujiingiza kwenye njia ya treni muda mfupi kabla ya saa 12:00 jioni (muda wa ujerumani).Utafanyika mkutano na waandishi wa habari kesho (leo) ili kutoa taarifa zaidi."
Enke, 32, amecheza mechi za kimataifa nane akiwa na timu ya taifa ya Ujerumani, na alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao wangeitwa kwenye kikosi cha Ujerumani kwa ajili ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Afrika Kusini.
Taarifa za kifo chake zimelishitua Shirikisho la Soka Ujerumani (DFB).
"Timu ya Ujerumani imeshitushwa na msiba huu mzito," ilisema taarifa ya DFB.
"Kocha wa timu ya taifa, Joachim Loew na Oliver Bierhoff, wote wameshtushwa na kifo hiki," ilisema zaidi taarifa hiyo.
Enke, aliwahi kucheza soka katika nchi za Hispania, Ureno na Uturuki kabla ya kusaini ligi ya Ujerumani 'Bundesliga' akiwa na timu ya Hanover mwaka 2004.

England yapata mashabiki lukuki 'Bondeni'

LONDON, England
WAYNE Rooney na wachezaji wenzake wa timu ya taifa ya England watashangiliwa na takribani mashabiki milioni 2.5 nchini Afrika Kusini Jumamosi wiki hii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya fainali za Kombe la Dunia Danny Jordan alikiri kuwa kikosi cha kocha Fabio Capello kitavuta wapenzi wengi nchini Afrika Kusini kufuatia mpambano wake huo na Brazil.
Jordaan alisema: "Afrika Kusini huenda ikawa ni wapenzi wakubwa wa soka la Uingereza duniani.
"Kila wiki tuna mechi tano za 'live' za Ligi Kuu ya England na kuna takribani mashabiki milioni 2.5 wanaounga mkono klabu za Ligi Kuu ya England.
"Nina uhakika wote watakuwa wakiiangalia England huku wakiwa wamevalia jezi za timu hiyo."Hilo lilitokea wakati England ilipocheza hapa mwaka 2003."
Karibu mashabiki 30,000 pia wanatarajiwa kusafiri kutoka England na kwenda Doha kwa ajili ya kushuhudia mchezo huo wa kirafiki.
David Beckham ni maarufu sana Afrika Kusini, na kwa mara nyingine tena anatarajiwa kuwa kivutio katika mashindano hayo yatakayofanyika katika kipindi cha majira ya joto endapo Capello atamchagua katika kikosi hicho.
Jordan aliongeza: "Mashabiki wa Chelsea watataka kumuona Terry na Lampard. Wakati mashabiki wa United nao watataka kumuona Rooney na wengine."
England ni moja kati ya majina makubwa katika soka duniani na wengi wanaipenda."Lakini Beckham ni jina kubwa zaidi hivyo atavutia watu wengi zaidi."

Ronaldo kuikosa Ureno

OBIDOS, Ureno

Cristiano Ronaldo, winga wa Ureno atakosa mechi mbili za kusaka nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Bosnia, lilisema Shirikisho la Soka la Ureno (FPF), katika taarifa yake jana.
Ronaldo hajapona maumivu yake ya kifundo cha mguu, na hatacheza mchezo utakaofanyika Lisbon Jumamosi na ule wa Zenica siku nne baadaye.
"Baada ya uchunguzi, imekubaliwa kuwa mchezaji huyo bado hajafikia kigezo vya kiafya kujiunga na timu ya taifa ya Ureno, "ilisema FPF.
Mchezaji huyo wa Real Madrid aliyesajiliwa kwa ada ambayo ni rekodi duniani, aliumia mwishoni mwa Septemba wakati Ureno ikishinda 3-0 dhidi ya Hungary na tangu wakati huo hajawahi kucheza.

Tuesday, November 10, 2009

Yanga yanyoosheana vidole

Na Jacqueline Massano, Jijini

Hali ya mvutano bado inaendelea ndani ya klabu ya Yanga, huku sasa wanachama wakitaka serikali kuingilia kati kuhusu tuhuma za ufujaji wa pesa ndani ya klabu hiyo kongwe nchini, na wakati huo huo wakitaka kuitishwa haraka kwa mkutano mkuu.
Mbali na kutaka kuingilia kati, pia wanataka watuhumiwa wote wa ufisadi wachukuliwe hatua za kisheria.
Baadhi ya wanachama walioongea na blog hii, wameulaumu uongozi kufuatia tuhuma za kupotea zaidi ya shilingi milioni 100 zilizotolewa na wanachama kwa ajili ya kadi.
Mmoja wa wanachama wa klabu hiyo na mchezaji wa zamani, Ramadhan Kampira (003925), alisema sasa imefika hali iliyopo ndani ya klabu ya Yanga haivumilika na serikali ni lazima iingiliea kati ili kunusuru.
Kampira amesema zaidi kuwa, 'utamaduni' wa ubadhilifu wa fedha Yanga sasa ni wa kawaida ndani ya Yanga.
"Kuna watu wachache wanaendelea kunufaika kwa jasho la wengine, nadhani muda umefika waondoke," alisema.
"Hapana sisi kama wanachama tumesema tumechoka, kwani suala la ufujaji wa fedha limekuwa ni tatizo sugu ndani ya klabu yetu. Hawa watafuna pesa za klabu wanaonekana mitaani na magari ya kifahari.
Nadhani mwenyekiti Iman Madega ana kila sababu ya kuitisha mkutano mapema ili kutoa taarifa ya mapato na matumizi tangu uongozi ulipoingia madarakani," aliongeza.
Naye mwanachama mwingine wa klabu hiyo, Omary Hussein ambaye pia aliwahi kuichezea klabu hiyo alisema serikali kupitia Wizara yake ya Michezo ni vyema ikaingilia kati suala la matumizi mabaya ya pesa za klabu ambazo wanachama wamezitoa kwa nia nzuri.
"Huu ni wizi, haiwezekani mtu kula fedha za wanachama kiulani tu, na ndiyo maana klabu yetu imeanza kudidimia kifedha na inashindwa kufanya vizuri, inaumiza sana," alisema.
Hata hivyo, Hussein alimtetea katibu mkuu wa kuajiliwa, Lawrence Mwalusako na kudai kuwa hausiki na tuhuma hizo za ufujaji wa fedha ndani ya klabu hiyo kwa sababu hana muda mrefu tangu aongoze klabu hiyo.
Hata hivyo, Mwalusako alikaririwa akidai kuwa yeye hafahamu chochote kuhusiana na upotevu wa fedha hizo ndani ya klabu hiyo, na kuwataka waandishi wamuulize aliyekuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Lucas Kisasa.

Liverpool yabanwa mbavu

LONDON, England

KIUNGO Steven Gerrard, jana aliiokoa kipigo Liverpool baada ya kupachika wavuni bao la kusawazisha lililotokana na penati ya utata dhidi ya 'vibonde' Birmingham City, na baada ya dakika 90, matokeo kuwa ya sare ya 2-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya England.
Nahodha Gerrard, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya nyonga, aliingia akitoka benchi la wachezaji wa akiba mwishoni mwa kipindi cha kwanza na kufunga bao la kusawazisha robo ya mwisho ya mchezo.
Penati hiyo ilitolewa baada ya Lee Carsley kumuangusha chini mchezaji wa Liverpool David Ngog, mfungaji wa bao la kwanza."Ni kama utani. Najua kwa ukweli kabisa sikumgusa," alisema Carsley wakati akiongea na ESPN
"Nadhani kama refa (Peter Walton) ataona tukio hili kwenye televisheni, hakika atasikitika sana."
Picha za televisheni zinaonyesha kuwa Carsley, ambaye alipewa kadi ya njano kwa kupinga adhabu hiyo, hakumgusa Ngog.
Liverpool ilionekana kama mambo yangekwenda mazuri baada ya kutangulia kufunga kwa bao la Ngog mapema, lakini mambo yalianza kwenda vibaya dakika ya 26 baada ya Christian Benitez kuisawazishia Birmingham.
Mambo yalikuwa mabaya zaidi baada ya Cameron Jerome kupiga shuti la umbali wa mita 30 na kumshinda kipa wa Liverpool Pepe Reina na kujaa wavuni.
Liverpool, inayoshika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, ilikuwa dimbani bila mshambuliaji wake mahiri Fernando Torres, ilicheza kwa nguvu baada ya mapumziko kujaribu kupata ushindi ili kupunguza pengo la pointi zinazofikia 11 dhidi ya wanaoongoza Chelsea.
Kocha Rafa Benitez ambaye kiti chake kina joto la 'kutimuliwa' kufuatia timu hiyo kufanya vibaya, aliokolewa na penati hiyo ambayo kama isingetinga wavuni, kingekuwa kipigo chake cha sita msimu huu.
"Nimeangalia picha ya televisheni, nadhani haikuwa penati," alisema Benitez wakati akiongea na BBC. "Inawezekana, lakini ukweli ni kwamba tuna wakati mgumu zaidi mwaka huu.
"Tulimiliki mpira kwa kiasi kikubwa na kufanya mashambulizi mengi langoni, lakini hatukuamini kwani mpaka mapumziko tulikuwa nyuma 2-1. Lakini hata hivyo, timu ilionyesha uwezo mkubwa."
Gerrard alicheza, lakini hakuwa fiti kwa asilimia 100. Bado alionyesha kiwango tulichohitaji kukiona," aliongeza Benitez.
Katika mechi hiyo, kiungo Alberto Aquilani alicheza kwa mara ya kwanza tangu ajiungea na klabu hiyo kutoka AS Roma Agosti.
Albert Riera na Yossi Benayoun waliongeza 'donda' la majeruhi Liverpool baada ya kuumia.Birmingham wanabaki katika nafasi ya 15 kati ya timu 20 zinazoshitiki ligi hiyo ikiwa na pointi 12.

Ruvu Shooting, Simba uso kwa uso

Na Jacqueline Massano, Jijini

TIMU ya Ligi daraja la kwanza ya Ruvu Shooting inatarajia kushuka dimbani kesho kumenyana na Simba katika mechi ya kirafiki inayotarajia kufanyika kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Akizungumza na blog hii jana, Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Pwani, Hassan Othman 'Hassanoo' amesema mechi hiyo itakuwa ni moja ya maandalizi kwa timu hizo mbili.
Amesema Ruvu Shooting ambayo imetinga hatua ya tisa bora katika mechi ya ligi daraja ya kwanza inajiandaa na hatua hiyo ili iweze kufanikiwa kupanda daraja na kucheza ligi kuu ya Tanzania Bara.
Hassanoo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Simba, amesema mechi hiyo itatumiwa na wekundu hao wa Msimbazi kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar.
Amesema kiingilio katika mechi hiyo kinatarajia kuwa sh. 5,000 kwa jukwaa kubwa, sh. 2,000 jukwaa la kijani na mzunguko sh. 1,000.

Keita 'out' siku 10


MADRID, Hispania
Kiungo wa Barcelona Seydou Keita ameshauriwa kupumzika kwa muda wa siku 10 baada ya kuumia goti.
Taarifa ya klabu hiyo--mabingwa wa vilabu barani Ulaya, ilisema jana kupitia tovuti yake (http://www.fcbarcelona.com/).
Keita aliumia wakati wa mechi ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Real Mallorca Jumamosi iliyopita, na anatarajia kuikosa mechi ya timu yake ya taifa ya Mali dhidi ya Ghana kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Aidha, ataikosa mechi ya Barcelona kuwania Kombe la Mfalme Jumapili wiki hii dhidi ya Cultural Leonesa.

Munucho aomba radhi Angola

LUANDA, Angola
Mshambuliaji wa Manucho, ambeya amesimamishwa kwa kuchelewa kuripoti kwenye kambi ya timu ya taifa, ameomba msamaha, taarifa kutoka Luanda zimethibitisha jana.
"Naomba radhi kwa kocha, wachezaji wenzangu na wananchi wote kwa ujumla," alisema kupitia chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali.
Angola, ambao ni wenyeji wa fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kuanzia Januari 10-30, ina mechi za kimataifa za kirafiki dhidi ya Congo na Ghana.
Kocha Manuel Jose alisema wiki iliyopita kuwa Manucho, mchezaji wa zamani wa Manchester United, na sasa anacheza Real Valladolid ya Hispania, hatocheza mechi za timu ya taifa vinginevyo aombe radhi.